1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS: Umoja wa Ulaya waunga mkono vikwazo dhidi ya Iran

13 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCSf

Umoja wa Ulaya umekaribisha uwezekano wa mazungumzo mapya ya kuutanzua mzozo wa nyuklia wa Iran. Hata hivyo umoja huo umesema utaendelea kuunga mkono vikwazo dhidi ya Iran kwa hatua yake ya kukataa kusitisha urutubishaji wa madini ya uranium.

Kiongozi wa shirika la kimataifa la kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia, Mohamed El Baradei, amesema vikwazo ni njia mojawapo ya kutuma ujumbe ulio wazi kwa Iran kupitia jumuiya ya kimataifa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba kuna wasiwasi kuhusu mpango wake wa nyuklia ambao bado haujaidhinishwa na shirika hilo.

El Baradei amesema vikwazo vitaondolewa kama Iran itatii agizo la baraza la usalama la Umfoja wa Mataifa.

´Nafikiri baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeweka wazi katika azimio lake kwamba ikiwa Iran itatii sharti la baraza hilo, vikwazo vitasitishwa. Na hiyo ndio maana watu wengi, mimi nikiwa mmoja wao, tunajaribu kutafuta njia ya kuacha kutegemea vikwazo badala yake tuelekee katika mazungumzo.´

Mawaziri wa Umoja wa Ulaya wanaokutana mjini Brussels, Ubelgiji wamesema mlango wa mazungumzo uko wazi lakini wakaidhinisha vikwazo vya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, ambaye nchi yake inashikilia urais wa Umoja wa Ulaya, amesema hawataki malumbano bali wanataka suluhisho lipatikane. Aidha Steinmeier amesema watafanya kila linalowezekana kulifikia lengo hilo.