1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS: Umoja wa Ulaya waanza mazungumzo ya uanachama wa Uturuki

26 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBo8

Umoja wa Ulaya leo umeanza tena mazungumzo ya uanachama wa Uturuki katika umoja huo mjini Brussels, Ubelgiji.

Mazungumzo hayo lakini yanatuwama juu ya maswala mawili ya uanachama ikiwa ni pamoja na takwimu na usimamizi wa fedha.

Ufaransa, ambayo rais wake mpya, Nicolas Sarkozy, anapinga uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya, ilikuwa imetishia kutumia kura yake ya turufu kutia munda kama Ujerumani ingeendelea mbele na mazungumzo kuhusu maswala muhimu ya sera ya kiuchumi na fedha.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeir, ameuonya Umoja wa Ulaya uheshimu ahadi zake katika mazungumzo ya uanachama wa Uturuki katika umoja huo.

´Kila mara kunapokuwa na haja ya mazungumzo ndani ya Umoja wa Ulaya ni utamaduni mzuri kutoikataa haja hii bali kwa pamoja kutafuta ufumbuzi. Vinginevyo nawahakikishieni tunabakia katika msimamo wa Ulaya wa kuzingatia sheria msingi na kuheshimu mikataba.´

Umoja wa Ulaya ulisitisha mazungumzo ya uanachama wa Uturuki mwishoni mwa mwaka jana kwa sababu ya mzozo wa kibiashara baina ya serikali ya mjini Ankara na Cyprus.

Wakati huo huo, waziri Frank Walter Steinmeier, amesema Croatia imo njiani kujiunga na Umoja wa Ulaya kama mwanachama wa 28.

Mazungumzo kuhusu uanachama wa Coratia yameanza katika sehemu sita mpya kati ya sehemu 35, ikiwa ni pamoja na mageuzi ya kisheria. Croatia inatumai kuwa mwanachama kamili ifikapo mwaka wa 2009.