1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BREMEN : Ulaya yaitaka Iran kuwaachilia wanamaji

31 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCDu

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanaokutana katika mji wa kaskazini wa Ujerumani Bremen wameitaka Iran kuwaachilia mara moja wanamaji 15 wa Uingereza waliotekwa na vikosi vya Iran wiki moja iliopita.

Katika rasimu ya taarifa mawaziri hao wameelezea kitendo hicho cha Iran kuwa sio halali.Wito huo unakuja ikiwa ni masaa machache tu baada ya televisheni ya Iran kuonyesha kile ilichokielezea kuwa kukiri kwa Nathan Thomas Summers mmojawapo wa wanamaji 15 wa Uingereza inaowashikilia kwa madai ya kuingia katika eneo la bahari yake.

Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair amelaani kuonyeshwa kwa mwanamaji huyo kwenye televisheni kuwa propaganda ya aibu.

Iran imeutaka Umoja wa Ulaya kutoingilia kati mzozo huo unaoendelea kati yake na Uingereza.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Mohammed al Hosseini amekaririwa na shirika la habari la serikali IRNA akisema viongozi wa Ulaya wanapaswa kujiepusha kuunga mkono uchokozi wa wanamaji wa Uingereza katika eneo la bahari yake.