1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brahimi akutana na Assad na wapinzani

25 Desemba 2012

Msuluhishi wa kimataifa Lakhdar Brahimi Jumatatu (24.12.2012 )ameelezea wasiwasi wake juu ya hali ya Syria baada ya kukutana na Rais wa nchi hiyo, Bashar al Assad pia amekutana na makundi ya upinzani ya ndani ya nchi.

https://p.dw.com/p/178vg
Assad akutana na Brahimi
Assad akutana na BrahimiPicha: Reuters

Ziara hiyo ya Brahimi mjini Damascus ni ya tatu kwa mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya Kiarabu aliepewa jukumu la kukomesha mzozo wa miezi 22 nchini humo ambapo baadhi ya waangalizi wanasema juhudi zake zimegonga ukuta.

Brahimi amekaririwa akisema baada ya kukutana na Assad kwamba wamebadilishana mawazo juu ya hatua zinazofaa kuchukuliwa kukomesha mzozo huo.Amesema Rais Assad ameelezea maoni yake na yeye amemjulisha juu ya kile alichokiona wakati wa mikutano yake mingi na viongozi wa nchi wakati wa ziara zake katika miji tafauti aliyoitemblea hivi karibuni pamoja na mazungumzo yake na maafisa wa serikali wa kanda.

Televisheni ya taifa imeulezea mkutano wao huo kuwa wa dhati ambapo Rais amemwambia Brahimi kwamba wanataka mafanikio ya juhudi zote ambazo pia zitalinda heshima na mamlaka ya Syria kujiamulia mambo yake.Brahimi amesema hali nchini Syria bado ni ya kutia wasiwasi na wanataraji kwamba makundi yote husika watachukuwa hatua ya kufikia ufumbuzi ambao unatarajiwa na wananchi wa Syria.

Hakuna mafanikio yaliyopatikana

Hakuna hatua kubwa iliofikiwa katika kukomesha mzozo huo tokea Brahimi ashike wadhifa huo hapo mwezi wa Septemba. Brahimi hapo Jumanne(25.12.2012)amekutana na makundi ya upinzani yalioko ndani ya Syria ambapo amekuwa na mazungumzo katika hoteli aliofikia mjini Damascus na ujumbe wa watu sita ukiongozwa na Hassan Abdel Azim mkuu wa Kamati ya Uratibu ya Taifa kwa Mabadiliko ya Kidemokrasia MCCDC ambalo ni kundi la upinzani linalovumiliwa na serikali.Ziara ya Brahimi nchini Syria inafanyika huku kukiwa na repoti kutoka gazeti moja la kila siku la Ufaransa kuhusu mpango wa Marekani na Urusi wa serikali ya mpito nchini Syria ambayo imezusha ghadhabu miongoni mwa wapinzani ambao wanapinga maafikiano yoyote yale na utawala wa sasa.Gazeti la Le Figaro limeripoti kwamba pendekezo la kuusuluhisha mzozo huo linahusu kuendelea kubakia madarakani kwa Assad hadi hapo mwaka 2014 lakini hatoruhusiwa kurefusha mamlaka yake baada ya hapo.

Brahimi akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na Assad.
Brahimi akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na Assad.Picha: Reuters

Mwanadiplomasia mmoja wa nchi za magharibi aliyeko Beirut amesema kwamba hiyo inaweza kuwa ziara ya mwisho ya Brahimi mjini Damascus iwapo hakuna maendeleo yoyote yale yatakayofikiwa kuutatua mzozo huo.Mwanadiplomasia huyo amesema juhudi za kuutatua mzozo huo wa Syria hazifiki popote kutokana na pande zote mbili, serikali na waasi, kugoma kuzungumza pamoja, na kwamba ufumbuzi utakuwa kwenye medani ya mapambano.

Mapambano yapamba moto kila uchao

Wanaharakati mjini Damascus wameliambia shirika la habari la dpa kwamba kumezuka mapambano kati ya waasi na vikosi vya Assad katika kitongoji cha Khaled Ibn al Walid. Shirika la Kuangalia masuala ya haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema umeme umekatwa kwenye mji huo mzima tokea Jumapili.Katika jimbo la kaskazini la Aleppo waasi wanadai kwamba ndege za kivita za serikali zilitumia gesi ya sumu wakati zilipoyashambuliamaeneo ya kitongoji cha Khalidiyeh.Mwanaharakati Abul Houda al- Homsi amesema watu 71 waliofikishwa hospitali walikuwa wakikabiliwa na matatizo ya kupumua na kichefuchefu.

Wapiganaji waasi nchini Syria.
Wapiganaji waasi nchini Syria.Picha: PHILIPPE DESMAZES/AFP/Getty Images

Katika mahojiano na kituo cha utangazaji cha Russia Today, waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Segei Lagrov, amesema itakuwa ni kujiuwa kisiasa kwa serikali ya Assad iwapo itatumia silaha za sumu dhidi ya upinzani.Amesema Assad amekuwa akiwahakikishia mara kwa mara kwamba hana mipango ya kutumia silaha hizo.

Mwandishi:Mohamed Dahman/dpa

Mhariri: Josephat Charo