1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Borussia Dortmund yaiadhibu FC Kolon kuifuata Hamburg

Sekione Kitojo
18 Septemba 2017

Borussia  Dortmund yakaa kileleni  mwa  Bundesliga baada  ya kuimwagia  kipigo  FC Kolon , lakini  malalamiko yatolewa  na  FC Kolon  kuhusu  bao la  pili.

https://p.dw.com/p/2kDbG
Deutschland Borussia Dortmund v Hertha BSC - Bundesliga
Kikosi cha Borussia DortmundPicha: Getty Images/Bongarts/M. Hitij

Mabingwa watetezi  wa  ligi  ya  Ujerumani Bundesliga  Bayern Munich  wameonesha  kwamba  wanania  ya kurejea  katika  nafasi yao  baada  ya  kuirarua  Mainz 05  kwa mabao  4-0  wakiwa  nyumbani , baada  ya  wiki  iliyopita  kuteleza na  kubugia  mabao 2-0  nyumbani  kwa  Hoffenheim. Kikosi  cha kocha Carlo Ancelotti  kilijisahihisha  na  kutoa  jibu  mjarabu  baada ya  wiki  ya  mtafaruku  ndani  ya  klabu  hiyo, ikiwa  wachezaji  mbali mbali  nyota wakitoa  matamshi ya  kutatanisha  kuhusu  mahusiano yao  na  kocha  na  pia  klabu  hiyo.

Deutschland Fußball Bundesliga- FC Bayern München - 1 FSV Mainz 05
Wachezaji Thomas Mueller na Robert Lewandowski wa Bayern Munich wakipongezana Picha: Reuters/M. Dalder

Robert  Lewandowski, Frank Ribery , Thomas Mueller na  pia  Arjen Robben walitoa maneno ya ama  malalamiko  ama  kukosoa  uongozi  wa  klabu. Licha  ya mtafaruku  huo wachezaji  wa  Bayern  waliweza  kuonesha uwanjani  kwamba  wao  ni  moto  wa  kuotea  mbali  na  kuirarua Club Anderlecht  ya  Ubelgiji  kwa  mabao 3-0  katika  mchezo  wa Champions League katikati ya  wiki.

Mlinzi  wa  Bayern Mats Hummels  alikuwa  na  haya  ya  kusema baada  ya  pambano  dhidi  ya  Mainz 05.

"Nafikiri , tumeridhika  na  nmchezo wa  leo. Bila  shaka ilikuwa ni hatua  tu  katika  njia  sahihi. Lakini hata  hivyo  ilikuwa  ni  jibu  la wazi , kwamba  siku ya  Jumanne  hakuna  kitu kitakachotuzuwia kufurahi. Nafikiri , mabao 4-0  katika mchezo  huo ni matokeo yanayostahili."

Deutschland  Borussia Dortmund - 1. FC Köln
Socratis na Aubameyang wa Dortmund wakifurahia baoPicha: picture alliance/dpa/I. Fassbender

Kwa  upande  wake Borussia  Dortmund  ambayo  katika  michezo minne  ya  Bundesliga  msimu  huu  mlango  wake  haujatikiswa , jana Jumapili  ilionesha  kwamba  inamedhamiria  msimu  huu  kuipa changamoto  Bayern  Munich  ambayo  ni  mabingwa  watetezi  na wanaowania  kunyakua  taji  hilo  kwa  mara  ya  sita  mfululizo. Borussia  Dortmund  inaongoza  katika  msimamo  wa  ligi  ikiwa suluhu kwa  pointi  na  Hannover 96 , lakini  ikiongoza  kwa  mabao.

Lakini  ushindi  wa  mabao 5-0 wa  Borussia  Dortmund  dhidi  ya FC Kolon , umeingia  doa  pale  Kolon  walipolalamikia  bao  la  pili  la Dortmund  kutokana  na  refa  kupiga  firimbi  kabla  mpira haujavuka msitari. Mwamuzi  aliashiria  kwamba  mchezaji  wa  Borussia Dortmund  alimsukuma  mlinda  mlango  wa  Kolon  na  hivyo  mpira kumponyoka na  ukasindikizwa  wavuni  na  mlinzi  wa  Dortmund Socratis. Refa  msaidizi  wa  video  alimfahamisha  mwamuzi kwamba  wachezaji  wa  Dortmund  hawakumgusa  mlinda  mlango Timo Horn  na  kwamba  hilo  ni  bao safi.

Deutschland Dortmund gegen Köln | Stöger Schmattke und Ittrich
Kocha wa FC Kolon Peter Stoeger(kushoto) na Schmattke mkurugenzi wa spoti wa FC Kolon wakijadiliana na refa wa mchezo huo IttrichPicha: picture alliance/AP Photo/M. Meissner

Bao hilo  linalalamikiwa  na  viongozi  wa  FC Kolon  kwamba aliwazuwia  wachezaji  wa  Kolon  kuzuwia  mpira  huo  kuingia wavuni. Lakini  hata  hivyo  inaonekana  dhahiri  kwamba  katika wakati mpira  huo  unaelekea  wavuni hakuna  mchezaji  wa  Kolon aliyekuwa  karibu  kuuondoa.

Tukio la  kusikitisha  lilitokea  katika  mchezo  kati  ya  Stuttgart  na Wolfsburg, ambapo mchezaji  wa  kati  wa  Stuttgart  Christian Gentner  aligongana  na  mlinda  mlango  wa  VFL Wolfsburg , na Gentner  kukutana  na  goti la  mlinda  mlago  huyo  moja  kwa  moja usoni na  kupoteza  fahamu na watoa  huduma ya kwanza walilazimika kushikilia  ulimi  wake ili  kunusuru  maisha  yake. Lakini madaktari  wanasema  hali  yake  inaendelea  vizuri hadi sasa. Mchezo huo ulimalizika kwa Wolfsburg  kukubali  kipigo  cha  bao 1-0. Kocha wa  Wolfsburg Andries  Jonker  ambaye  nae  baada  ya matokeo  mabaya  ya  timu  hiyo  amefutwa  kazi  hii  leo, amesema baada  ya  pambano  hilo  kuwa  tukio  hilo halikuleta sura  nzuri katika  mchezo  huo.

Deutschland VfB Stuttgart - VfL Wolfsburg 1:1
Christian Gentner akipatiwa matibabu uwanjani baada ya kugongana na mlinda mlango wa Wolfsburg Picha: picture alliance/Avanti-Fotografie/R. Poller

"Kwa kweli  huo ni  wakati wa kutisha , wakati  mlinda  mlango akitoka kuufuata  mpira, na  unafahamu , kwamba  wakati  wowote kitu chochote kinaweza  kutokea, kwamba  kunaweza  kutokea mgongano. Lakini  unamatumaini  kila  mara , kwamba  hakuna mchezaji  atakayeumia , bila  shaka  hakuna  mlinda  mlango  ama mchezaji wa  ndani. Hali hiyo si  nzuri."

Hannover 96 inayoshika  nafasi  ya  pili  baada  ya  Borussia Dortmund  katika  msimamo  wa  ligi  ya  Ujerumani Bundesliga imeendeleza  ushindi  siku  ya  Jumamosi  baada  ya  kuikandika Hamburg SV  kwa  mabao 2-0 siku  ya  Ijumaa , ambapo ilishika nafasi  ya  uongozi japokuwa  kwa  muda  tu kwa  mara  ya  kwanza tangu  Neil Amstrong  wa Marekani  kutua  mwezini  miaka  48 iliyopita.

FC Schalke 04  iliibwaga  Bremen  kwa  mabao  2-1  na  kocha  wao kijana  Domenico  Tedesco  amesema mchezo  huo hata  kama ungemalizika  kwa  sare  asingelalamika.

DFB -Pokal BFC Dynamo vs. FC Schalke 04 Domenico Tedesco Trainer
Domenico Tedesco kocha wa Schalke 04Picha: Reuters/A. Schmidt

"Kwa ukweli, mchezo  huo  ungemalizika  kwa  sare  ya  mabao 2-2. Lakini  tumefurahi  na tumeridhika  kwa  kunyakua  pointi  zote  tatu na  tunawatakia  Bremen  bila  shaka  katika  mchezo  ujao  kila  la kheri."

RB Leipzig yatunisha misuli

RB Leipzig  baada  ya  kuonesha  misuli  yake  wiki  iliyopita  dhidi ya  Freiburg  , ilishikwa  shati  pale  ilipotoka  sare  ya  mabao 2-2 na  Boruusia  Moenchengladbach. Wakati  Bayer Leverkusen  chini ya  kocha  wao  mpya  Heiko Herlisch  ilipata  ushindi  wake  wa kwanza  msimu  huu  baada  ya  kuirarua  Freiburg  kwa  mabao 4-0.

Fußball Bundesliga RB Leipzig - Borussia Mönchengladbach
Timo Werner wa Leipzig katikati akipenya katika ngome ya MoenchengladbachPicha: picture-alliance/dpa/J. Woitas

Hoffenheim ikatoka  sare  ya  bao 1-1  na  Hertha BSC Berlin.

Kocha Andries Jonker  amekuwa  kocha  wa  kwanza  katika Bundesliga  kibarua  kuota nyasi msimu  huu, baada  ya  Wolfsburg kuamua  kutengana  nae leo baada  ya  kupata  pointi  nne  tu  katika michezo  minne  ya  Bundesliga.

Kocha  huyo  mwenye  umri  wa  miaka  54 raia  wa  Uholanzi alichukua  hatamu  za  kuiongoza  klabu  hiyo Februari  mwaka  huu, baada  ya  kuacha  kazi  ya  mkufunzi  mkuu  wa  kituo  cha  vijana wa  klabu  ya  Arsenal  London  na  kufanikiwa  kuibakisha Wolfsburg  katika  ligi  ya  Ujerumani  Bundesliga  msimu  uliopita, lakini  kipigo  cha  bao 1-0 siku  ya  Jumamosi  dhidi  ya  VFB Stuttgart  kilikuwa  ni  uthibitisho  wa  mwisho  kwamba  ndoa  hiyo haiwezi  tena  kuendelea.

Deutschland Bundesliga Andries Jonker und Martin Schmidt
Andries Jonker (kushoto) akisalimiana na kocha wa zamani wa Mainz 05 Martin Schmidt ambaye anachukua nafasi yake baada ya kufutwa kazi na VFL WolfsburgPicha: imago/Sven Simon

Jonker afutwakazi

Jonker  hata  hivyo  si  peke  yake , kwani  katika  Premier  League nchini  Uingereza, kwani  kocha  wa  Club Anderlecht  ya  Ubelgiji Rene Weiler  amepoteza  kazi  baada  ya  klabu  hiyo  kuanza  kwa kusuasua  msimu  huu. Kufukuzwa  kazi  kwa  Weiler  kulitangazwa siku  mbili  baada  ya  mashabiki  wa  klabu  hiyo  kuandamana  nje ya  uwanja  wakitaka  kocha  huyo  aondolewe  kufuatia  kikosi chake  kutoka  sare  ya  mabao  2-2 dhidi  ya  timu  ya  chini  ya Kortrijk siku  ya  Jumamosi. Rene Weiler  alishinda  mataji  34 na klabu  hiyo , na  kufikia  robo  fainali  ya  ligi  ya  Ulaya , kufuzu kuingia  katika   awamu  ya  makundi  ya  Champions League  na kuwatoa  vijana  wengi  kutoka  akademi  ya  klabu  hiyo kama  Youri Tielemans na  Leander Dendoncker, klabu  hiyo  imesema  katika taarifa.

Ligi yarejea tena viwanjani

Timu inayoongoza ligi ya  Ujerumani  Bundesliga  Borussia  Dortmund na  mabingwa  watetezi  Bayern  Munich  wanarejea  viwanjani  tena katikati  ya  wiki  kuweza  kuweka  msukumo  zaidi  katika  ushindi wao  wa  mwishoni  mwa  juma. Borussia  Dortmund  inasafiri kwenda  kupambana  na  Hamburg SV  siku  ya  Jumatano , masaa 24  baada  ya  Bayern  kukumbana  na  Schalke  04  kesho Jumanne.

Fußball Bundesliga Eintracht Frankfurt - FC Augsburg
Wachezaji wa Werder Bremen Picha: Getty Images/Bongarts/M. Hangst

Kwa  upande  mwingine  wa  msimamo  wa  ligi FC Kolon, Werder  Bremen  na  Freiburg  zitahitaji  kupata  ushindi  wao  wa kwanza. FC Kolon  inapambana  na  Eintracht Frankfurt , wakati Borussia  Moenchengladbach  ina  miadi  na  Stuttgart. Augsburg inataka  kuendeleza  uwezo  wake  wa  kushinda  msimu  huu itakapopambana  na  RB Leipzig  na Wolfsburg  ambayo  itafunzwa hivi  sasa  na  kocha  Martin Schmidt itajaribu  bahati  yake  dhidi  ya Bremen. Hertha  inakutana  na  Leverkusen  siku  ya  Jumatano  na Mainz  inaikaribisha  Hoffenheim  siku  ya  Jumatano.

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / dpae / ape / rtre / afpe

Mhariri: Yusuf , Saumu