1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Borussia Dortmund washika usukani wa Bundesliga

20 Februari 2012

Mabingwa watetezi Borussia Dortmund wamechukua usukani katika kinyang'anyiro cha ligi ya soka Ujerumani Bundesliga huku msimu ukijiandaa kuingia katika awamu ya tatu na ya mwisho

https://p.dw.com/p/14654
Kikosi cha Borussia Dortmund
Kikosi cha Borussia DortmundPicha: dapd

Wakati Dortmund wakipepea, mahasimu wao Bayern Munich nao watahitaji kujiangalia katika kioo kwa muda mrefu kutokana na matokeo yao duni ya hivi karibuni.

Klaas-Jan Huntelaar alifunga magoli mawili na kuisaidia Schalke kuwazaba Wolfsburg magoli manne kwa nunge. Huntelaar sasa anaongoza kwa pamoja na mshambuliaji wa Bayern Munich Mario Gotze kwa ufungaji mabao wakiwa na 18 kila mmoja. Hannover iliwafunga Stuttgart 4-2. Schalke sasa iko nyuma ya Bayern kwa pointi moja katika nafasi ya nne. Bayern ilianguka katika nafasi ya tatu baada ya sare ya bila kufungana na Freiburg ambao wanashikilia mkia. Borussia Dortmund wanaongoza na faida ya pointi tatu mbele ya Borussia Moenchengladbach

Chelsea kuiwakilisha Uingereza katika Champions League

mechi za Ligi ya Mabingwa barani Ulaya – UEFA Champions League, Chelsea ambao wanaonekana kuishiwa motisha watasafiri hadi Italia kumenyana na Napoli Jumanne usiku. Chelsea inatazamiwa kuwa klabu ya pekee iliyosalia kuiwakilisha Uingereza katika dimba hilo baada ya Manchester United na Manchester City kuteremshwa hadi kombe la Europa League, nao Arsenal wanaonekana kukaribia kuondolewa kutoka dimba hilo la mabingwa. Wakati kocha wa Chelsea Andre Villas - Boas akikiri kupoteza uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya wachezaji wake, Napoli imejawa na ujasiri baada ya kuwazaba Fiorentina magoli matatu kwa sifuri siku ya Ijumaa.

Wachezaji wa Chelsea wakisheherekea goli lao
Wachezaji wa Chelsea wakisheherekea goli laoPicha: picture-alliance/dpa

Nao mabingwa mara tisa Real Madrid watakuwa nchini Urusi kukabiliana na CSKA Moscow. Mabingwa wa zamani Inter Milan na Marseille watakutana Jumatano wakati Bayern Munich wakipambana na FC Basel.

Chisora huenda akapigwa marufuku ya maisha

Bondia wa uzani wa juu Dereck Chisora huenda akakabiliwa na adhabu ya kupigwa marufuku ya maisha baada ya vurumai zilizozuka kati yake na hasimu wake Muingereza David Haye baada ya mkutano wake na waandishi habari. Katibu mkuu wa Bodi ya Udhibiti wa Ndondi nchini Uingereza Robert Smith ameiambia BBC Radio 5 Live kuwa Chisora anaweza kupigwa marufuku ya maisha. Alisema bodi hiyo ina mamlaka mengi, inaweza kutoza faini, inaweza kumsimasha mwanabondia, na inaweza kumpokonya leseni.

Bondia wa uzani wa juu Muingereza Dereck Chisora
Bondia wa uzani wa juu Muingereza Dereck ChisoraPicha: picture alliance/dpa

Polisi wa Ujerumani bado haijazungumza na David Haye baada ya kutoweka kufuatia matukio hayo ya ghasia katika ukumbi ya Olympiahalle. Smith amesema wameanzisha uchunguzi kuhusiana na tukio hilo na kisha kumchukulia hatua za kinidhamu Chisora kwa sababu ni mwanabondia aliye na leseni. Kwa sasa Haye hana leseni ya ubondia kwa sababu tayari amestaafu.

Chisora alirejea nchini Uingereza kutoka Ujerumani Jumapili jioni baada ya kurushiana maneno mazito na Haye na hata Chisora akatishia kumpiga risasi na kumchoma moto Haye. Chisora alishindwa na bingwa mtetezi Vitali Klitschko kwenye pigano la Jumamosi la uzani wa juu taji la WBC mjini Munich, na akazuiliwa na polisi pamoja na mkufunzi wake Don Charles katika uwanja wa ndege ambapo walihojiwa.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman