Bomba la mafuta lalipuliwa Homs | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.02.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Bomba la mafuta lalipuliwa Homs

Nchini Syria kumefanyika hujuma kwenye bomba la mafuta na kusababisha moto mkubwa katika mji wa Homs ambao kwa wiki mbili zilizopita umeshuhudia kiwango kikubwa cha ghasia na operesheni za jeshi la serikali.

Moshi mweusi kutoka kwenye bomba lililolipuliwa mjini Homs

Moshi mweusi kutoka kwenye bomba lililolipuliwa mjini Homs

Kulingana na ripoti ya shirika la ukaguzi wa haki za binadamu nchini Syria (Syrian Observatory for Human Rights) lenye makao mjini London Uingereza, bomba hilo la mafuta lililolipuliwa liko katika eneo la Baba Amr ambalo linadhibitiwa na waasi. Kwa muda wa siku 12 zilizopita eneo hilo limekuwa likitwangwa kwa makombora yanayorushwa na vikosi vya serikali. Shirika hilo pia limearifu kuwa mji wa Hama ambao nao ni ngome ya upinzani umeshambiliwa na jeshi la serikali, na mawasiliano ya simu na mtandao wa internet yamekatwa.

Picha za video zilizowekwa kwenye mtandao na wanaharakati wa upinzani katika mji wa Homs, zimeonyesha moshi mkubwa mweusi ukifuka kutoka sehemu ambayo inaonekana kuwa makazi ya watu. Syria inavyo viwanda viwili vya kusafisha mafuta, na kimojawapo kiko katika mji wa Homs.

Rais Bashar al Assad wa Syria

Rais Bashar al Assad wa Syria

Mgogoro wa zaidi ya miezi kumi sasa nchini Syria ulianza kama maandamano ya amani kupinga utawala wa mabavu wa Rais Bashar al Assad, lakini sasa umechukua sura mpya ya mapambano ya kivita kati ya vikosi vya serikali na waasi waliojihami kwa silaha. Kumeripotiwa pia msako na kukamata watu katika mtaa wa Barzeh wa mjini Damascus.

Kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na haki za binadamu kimesema wiki hii kuwa watu zaidi ya 5,400 waliuawa nchini Syria mwaka jana, na kwamba idadi ya vifo na majeruhi inaongezeka kila kukicha. Mkuu wa kitengo hicho Navi Pillay alisema matendo ya serikali ya Damascus ni uhalifu dhidi ya binadamu, na kwamba maafisa wanaohusika walikuwa wakitayarisha mashtaka dhidi yake katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC.

Mkurugenzi wa shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch Kenneth Roth anakubaliana na msimamo huo wa Umoja wa Mataifa.

''Nadhani kiwango cha mashambulizi ambacho tumekishuhudia katika mji wa Homs, hususan mnamo wiki mbili zilizopita, ni kukithiri kwa matumizi ya nguvu kukandamiza upinzani. Kwa hivyo, wito kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu kuingilia kati ni muhimu sana kwa sasa. Bila shaka huu ni uhalifu dhidi ya binadamu unaoendeshwa na vikosi vya serikali.'' Alisema Kenneth Roth.

Kura za turufu za Urusi na China ziliuzuia Umoja wa Mataifa kupitisha azimio juu ya Syria

Kura za turufu za Urusi na China ziliuzuia Umoja wa Mataifa kupitisha azimio juu ya Syria

China ambayo ilitumia kura yake ya turufu kusimamisha azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya Syria, imetoa wito wa kufanyika mazungumzo kati ya serikali na wapinzani kumaliza tofauti zao kwa njia ya amani.

Akiongea mjini Washington, naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa China Cui Tiankai, amesema ni muhimu kuanzishwa kwa mazungumzo yanayozileta pamoja pande zinazohasimiana nchini Syria.

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE/AFP

Mhariri:Abdul-Rahman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com