Blair anafaa kuwa mpatanishi katika Mashariki ya Kati? | Magazetini | DW | 27.06.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Blair anafaa kuwa mpatanishi katika Mashariki ya Kati?

Kutoka magazeti ya hapa Ujerumani ya leo hii, kuna mada mbili. Moja ni jukumu jipya la waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair anayeondoka madarakani leo kama mpatanishi katika utaratibu wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati. Na la pili ni kesi ya kijana wa Kijerumani aliyekamatwa Uturuki na ambayo imezusha hata mvutano wa kidiplomasia kati ya Ujerumani na Uturuki.

Tukianza na suala la Tony Blair lakini, gazeti la “Frankfurter Allgemeine” linatathmini umuhimu wa mwakilishi maalum kwa Mashariki ya Kati. Limeandika:

“Hata ikiwa ni muhimu kuwa na mpatanishi, ni juu ya wahusika wenyewe hasa kutafuta suluhisho na kupata amani. Mkutano wa juzi mjini Sharm-el-Sheikh utaweza kuleta mafanikio tu ikiwa pande zote zinazohusika katika mzozo huu zitakubaliana – bila ya au pamoja na Tony Blair. Tusisahahu kupatikana amani katika Mashariki ya Kati kulikuwa lengo muhimu la waziri mkuu huyu anayestaafu, licha ya matokeo ya Iraq.”

Mhariri wa gazeti la “Nordkurier” ana wasiwasi juu ya Blair kuwa mpatanishi katika eneo la Mashariki ya Kati:

“Bila shaka, waziri mkuu huyu alionyesha kuwa anaweza kuitatua mizozo kama ule wa Irland ya Kaskazini. Lakini hiyo haitamsaidia katika Mashariki ya Kati. Huko sifa ya Tony Blair imevunjika kwa sababu ya kuiunga mkono Marekani katika vita vya Iraq na pia kutokana na kukataa kwake kuunga mkono makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na Libanon mapema. Hayi si vielelezi vya mpatanishi mzuri.”

Tuende sasa kwa maoni ya wahariri juu ya kesi ya kijana wa Kijerumani mwenye umri wa miaka 17 ambaye alikamatwa Uturuki kutokana na tuhumu za kumwingilia kimapenzi msichana wa miaka 13. Kama tulivyosikia katika ripoti, waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, anataka kijana huyu aachiliwe huru, wakati serikali ya Uturuki inasisitiza juu ya uhuru wa mfumo wake wa sheria. Juu ya mvutano huu, gazeti la “Kölner Stadtanzeiger” limeandika:

“Wanasiasa wa Ujerumani wanatumia wakati huo ambapo hamna habari nyingine muhimu kujipatia sifa nzuri, lakini kwa kweli wanajipatia sifa ya kipumbavu. Kwani hakimu wa hapa nchini hangekubali kumuachilia mshtakiwa ikiwa angeambiwa kufanya hivyo na waziri mkuu au mwanasiasa yeyote mwingine wa Uturuki. Basi, kama serikali ya Uturuki sasa inasisitiza, mfungwa huyu wa Kijerumani hatakuwa tofauti, ni msimamo unaofahamika kabisa.”

Ni gazeti la “Kölner Stadtanzeiger”. Mhariri wa “Berliner Tagesspiegel” anakosoa namna kisa hiki kinavyozungumziwa humu nchini. Ameandika:

“Kijana wa Kijerumani ambaye ni mhanga wa maamuzi yasiyokuwa na msingi na tamaduni za zamani za Kituruki amefungwa katika gereza mbaya sana – hiyo ndiyo picha inayotumika. Wanasiasa kama waziri mkuu wa jimbo la Lower Saxony anasema kisa cha kijana huyu ni kama ishara ya tofauti kubwa kati ya Ujerumani na Uturuki. Ikiwa tunaweza kuutumia mfano huu, kwa kweli inaonyesha tofauti kati ya Ujerumani na Uingereza. Kwani alikuwa ni mtalii wa Kiingereza ambaye alimshutumu kijana huyo akiwa na wasiwasi juu ya binti yake.”

 • Tarehe 27.06.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHSa
 • Tarehe 27.06.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHSa