1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden kukutana na viongozi wa Ukraine

21 Novemba 2014

Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden leo (21.11.2014) atakutana na viongozi wa Ukraine, ikiwa ni mwaka mmoja tangu kuanza maandamano yaliyomuondoa madarakani Rais wa Ukraine Viktor Yanukovich, aliyeungwa mkono na Urusi.

https://p.dw.com/p/1Dqvb
Rais Petro Poroshenko na Joe Biden
Rais Petro Poroshenko na Joe BidenPicha: Reuters

Joe Biden aliyewasili mjini Kiev jana, hii leo atakutana na Rais Petro Poroshenko na Waziri Mkuu, Arseniy Yatsenyuk, ambao wanatarajia kuwa kiongozi huyo wa Marekani atasisitiza nia ya nchi yake kutoa msaada zaidi wa kupambana na wapiganaji wa mashariki mwa Ukraine.

Mwezi Septemba, Marekani ilitoa msaada wa Euro milioni 42, ili kuimarisha usalama nchini Ukraine. Hata hivyo, Urusi ambayo imekuwa ikishutumiwa kwa kuuchochea mzozo wa Ukraine, imeonya hatua ya Marekani kulisaidia jeshi la Ukraine itauchochea zaidi mzozo kwenye eneo hilo.

Katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la Ukraine la The Day na kuchapishwa siku ya Alhamisi (20.11.2014), Biden ambaye ni kiongozi wa juu kutoka nchi za Magharibi kuzuru Ukraine hivi karibuni, alisisitiza kuwa hakuna suluhisho la kijeshi katika mzozo wa Ukraine na ameishutumu Urusi kwa kuingilia masuala ya ndani ya Ukraine ambalo ni taifa huru.

Waziri Mkuu wa Ukraine, Arseniy Yatsenyuk
Waziri Mkuu wa Ukraine, Arseniy YatsenyukPicha: Reuters

Biden alisema anapeleka ujumbe muhimu wa kuwaunga mkono watu wa Ukraine na serikali na kwamba atazungumza zaidi baada ya kuwasili Kiev.

Watu wapatao 1,000 wauawa

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umesema kuwa kiasi cha watu 1,000 wameuawa nchini Ukraine tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yalipofikiwa mwezi Septemba mwaka huu mjini Minsk, Belarus, kati ya serikali na waasi wanaotaka kujtenga kwa eneo la mashariki mwa Ukraine.

Shirika la Haki za Binadaamu la Umoja wa Mataifa limesema kuwa kiasi cha watu 13 hufariki dunia kila siku katika mzozo huo. Ujumbe wa shirika hilo nchini Ukraine, umesema watu 957 waliuawa kati ya Septemba 5 makubaliano yaliposainiwa hadi Novemba 18, mwaka huu.

Kamishna wa Shirika la Haki za Binadaamu la Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein, amesema idadi ya waathirika inazidi kuongezeka. Amesema raia, wakiwemo wanawake, watoto, watu wachache na watu wanaoishi katika mazingira magumu, wanaendelea kuteseka kutokana na mzozo wa kisiasa wa Ukraine. Katika ripoti yake, shirika hilo pia limeelezea kuhusu ukiukwaji wa haki za binaadamu uliofanywa na pande zote zinazohusika.

Zeid Ra'ad Zeid Al-Hussein
Zeid Ra'ad Zeid Al-HusseinPicha: Mike Coppola/Getty Images for Kairos Society

Ama kwa upande mwingine, ujumbe wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, OSCE, uliopo nchini Ukraine, umesema moja ya timu zake ilishambuliwa na mtu aliyekuwa na sare. OSCE, ina waangalizi wapatao 300 nchini Ukraine, kufatilia mkataba wa kusitisha mapigano ambao umesitisha mapigano kwenye maeneo mengi ya mzozo, lakini umeshindwa kuzuia mashambulizi katika maeneo hatari.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef