1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bibiana Steinhaus aweka historia Bundesliga

Bruce Amani
11 Septemba 2017

Mjerumani Bibiana Steinhaus ameweka historia ya kuwa refarii wa kwanza mwanmke kuongoza mchuano katika ligi ya daraja juu barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/2jjOs
Bundesliga Berlin vs Bremen
Picha: picture-alliance/AP/M. Sohn

Steinhaus mwenye umri wa miaka 38, ni mwanamke wa kwanza kuongoza mechi katika ligi kuu ya Bundesliga, kitu ambacho hakijawahi kutokea katika ligi England, Ufaransa, Italia wala Uhispania. Alikuwa na ujuzi wa kutosha kutokana na mechi 80 alizoongoza katika ligi ya daraja ya pili tangu mwaka wa 2007 na mara kadhaa alikuwa kama refarii msaidizi katika Bundesliga, lakini jana ilikuwa mchezo wake wa kwanza akiwa refarii katika ligi kuu.

Bundesliga Berlin vs Bremen Bibiana Steinhaus
Steinhaus amepongezwa kwa kufanya kazi nzuriPicha: picture-alliance/dpa/S. Stache

Klabu ya Hertha Berlin ilipunguza kwa nusu tikiti za mashabiki wa kike ambao walitaka kumwona Steinhaus akiendesha shughuli uwanjani Berlin. Mechi ilienda sawa kabisa na akamiminiwa sifa na kutoka kila upande. Rais wa shirikisho la kandanda la Ujerumani DFB Reinhard Grindel alisema Steinhaus alikuwa chini ya shinikizo kubwa lakini alistahili hilo na kufanya maamuzi mazuri katika mtanange huo.

Katika mechi nyingine ya jana, Schalke ilifunga mabao mawili katika dakika moja baada ya kipindi cha mapumziko na kupata ushindi wa mabao matatu kwa moja nyumbani dhidi ya Stuttgart. Matokeo hayo yameiweka Schalke katika nafasi ya tano, mbele ya mabingwa watetezi Bayern Munich, ambao wako katika nafasi ya sita baada ya kuduwazwa Jumamosi na Hoffenheim.

Ushindi wa Hoffenheim wa 2-0 dhidi ya Bayern ni wa pili mfululizo nyumbani dhidi ya Bayern uliosimamiwa na kocha chipukizi Julian Nagelsmann. Bayern ilikuwa ilishambulia lango la Hoffenheim mara 23 bila mafanikio.

Fußball TSG 1899 Hoffenheim v FC Bayern München - Bundesliga
Bayern Munich waliutawala mchezo lakini wakachapwaPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Wakati huo huo, Freiburg iliusitisha mwanzo mzuri wa Borussia Dortmund msimu huu, baada ya kulazimisha sare ya 0-0.

Mabeki wa BVB Marc Bartra na Marcel Schmelzer waliondolewa uwanjani katika kipindi cha kwanza baada ya kuumia. Kiungo Mfaransa Yoric Ravat alilishwa kadi nyekundu baada ya kumchezea visivyo Bartra.

Katika matokeo mengine Eintracht Frankfurt ilipata ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Borussia Moenchengladbach wakati Augsburg iliinyeshea Cologne tatu bila. Mainz ilitoka nyuma na kuifunga Bayer Leverkusen 3-1 nao Wolfsburg wakatoka sare ya 1-1 na Hannover

Rummenige amjibu Lewandoski

Mwenyekiti wa Bayern Munich Karl-Heinz Rummenige amemjibu Robert Lewandowski baada ya mshambuliaji huyo wa Poland kuikosoa sera ya usajili wa wachezaji wapya ya miamba hao wa Bavaria. Lewandoswki hivi karibuni alisema katika mahojiano na gazeti la Bild hapa ujerumani kuwa Bayern wanakabiliwa na kitisho cha kuachwa nyuma na vilabu vikuu barani Ulaya, akitoa mfano wa PSG. SRummenige amesema "Lewandowski ameajiriwa na Bayern kama mcheza kandanda, na analipwa hela nyingi sana, nimekasirishwa na kauli zake”.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP
Mhariri: Yusuf Saumu