1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biashara ya silaha kwa Afrika

Oumilkher Hamidou16 Machi 2010

Taasisi inayosimamia masuala ya amani SIPRI inaonya dhidi ya kuongezeka biashara ya silaha nchini Afrika kusini na Algeria

https://p.dw.com/p/MU42
Nyambizi za Ujerumani ni miongoni mwa silaha zinazonunuliwa na Afrika kusiniPicha: picture alliance / dpa

Mayowe yalihanikiza nchini Ujerumani jana pale ripoti ya taasisi ya kimataifa inayochunguza masuala ya amani SIPRI ilipozungumzia juu ya kuzidi biashara ya silaha ya Ujerumani.Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita,biashara ya silaha ya Ujerumani imeongezeka zaidi ya mara dufu.Wanunuzi wanakutikana bila ya shaka pia barani Afrika ambako ugavi na utashi vinazidi kuongezeka.

Algeria na Afrika Kusini,kwa mujibu wa taasisi ya mjini Stockholm ya SIPRI ndizo wanunuzi wakubwa wa silaha.Fedha zinazotolewa na nchi hizo mbili kwa pamoja kwaajili ya kununua silaha zinafikia thuluthi mbili ya fedha jumla za biashara ya silaha barani Afrika.Hata hivyo sababu zinazoyafanya madola hayo mawili makuu kiuchumi barani Afrika kuagizia silaha ni tofauti toka nchi moja hadi nyengine.Algeria yenye utajiri wa mafuta tokea hapo imejijenga kijeshi na inahasimiana na jirani yake Moroko.

Afrika kusini kwa upande wake,kwa mujibu wa Pieter Wezeman wa taasisi ya SIPRI inalenga zaidi kuigeuza iwe ya kisasa shehena yake ya silaha.Hata hivyo mtaalam huyo anastaajabishwa na kiwango kikubwa cha fedha kinachotolewa na Raas ya matumaini mema kwaajili ya kununua silaha.

"Hapo bila haka linazuka suala,kama fedha zinazotolewa si nyingi mno?Mtu anaweza kwa mfano kujiuliza:Kwanini Afrika kusini inanua nyambizi kutoka Ujerumani.Kusema kweli hakuna jirani yeyote anaemiliki manuari za kijeshi katika eneo hilo.Kwa hivyo wanalenga kitu gani?"

Katika eneo la kaskazini mwa Afrika,gharama za kijeshi ni kubwa mno zikilinganishwa na pato la ndani la nchi za eneo hilo-katika baadhi ya nchi gharama hizo zinafikia asili mia tano ya pato la ndani.

Kusini mwa jangwa la Sahara picha inayojitokeza ni afadhali kidogo,ikitengwa bajeti inayotisha ya silaha nchini Eritrea.

Haimaanishi lakini kwamba katika eneo hilo hakuna matumizi ya nguvu au silaha,anasema Guy Lamb wa taasisi ya Afrika kusini inayoshughulikia masuala ya usalama.Anazungumzia juu ya mapanga na silaha ndogo ndogo zilizokua zimeenea kwa mfano nchini Rwanda katika miaka ya 90 na kusababisha malaki ya watu kuuliwa.

Anasema ikiwa silaha ndogo ndogo zitaachiwa kuingia katika maeneo ya mizizo,basi bila ya shaka matokeo yake yatakua kuongezeka matumizi ya nguvu.

Umoja wa mataifa unajaribu kuepusha hali hiyo istokee kwa kuzipiga marufuku silaha hizo katika maeneo hayo.Kwasasa kuna marufuku sabaa ya silaha,miongoni mwa maeneo ambako marufuku hayo yametangazwa ni Darfour nchini Sudan.Hata hivyo nchi na mashirika kila wakati yanajipatia njia za kukiuka marufuku hayo.

Mwandishi :Adrian Kriesch/Hamidou Oummilkheir

Imepitiwa na Saumu M.Ramadhan.Yusuf