1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bhutto auawa katika shambulizi la kujitoa mhanga

27 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/Ch6c

RAWALPINDI.Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Pakistan, Bi Benazir Bhutto ameuawa katika shambulizi la bomu la kujitoa mhanga mara baada ya kuhutubia mkutano wa kampeni katika mji wa Rawalpindi.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Pakistan imethibitsha kuwa Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Pakistan amekufa kutokana na majeraha aliyoyapata kutokana na shambulizi hilo.

Msemaji wa chama cha Bi Benazir Bhutto Rehman Maliki amethibitsha kuawa kwa Waziri Mkuu huyo wa zamani.

Shambulizi hilo lilitokea baada ya Bi Bhutto aliyekuwa na umri wa miaka 54 kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara kuelekea uchaguzi wa tarehe 8 mwezi ujayo, ambapo inaarifiwa kuwa watu wengine 20 wameuawa wakiwemo askari polisi.

Taarifa zinasema kuwa Bi Bhutto ameuawa kwa risasi zilizofyatuliwa kuelekea kwenye gari yake wakati anaondoka kwenye mkutano huo ambapo zilimpiga shingoni na kifuani, na muda mfupi baadaye kukatokea mlipuko huo.

Miezi miwili iliyopita wakati alipokuwa akirejea nyumbani kutoka uhamishoni, msafara wake ulishambuliwa na bomu la kujitoa mhanga ambapo watu zaidi ya mia moja waliuawa.

Waziri Mkuu mwengine wa zamani wa nchi hiyo Nawaz Shariff amelaani shambulio hilo na kusema linayaweka pabaya majaaliwa ya Pakistan.

Amesema kuwa ni mungu pekee ndiyo anayejua vipi nchi hiyo itakabiliana na ghadhabu za wananchi kuhusiana na mauaji hayo.

Wakati huo huo mataifa mbalimbali duniani yamelaani shambulizi hilo, ambapo nchini Marekani, nchi hiyo imesema kuwa shambulizi hilo limeonesha kuwa bado kuna watu wasiyotaka maendeleo katika mpango wa maridhiano na demokrasia.

Urusi nayo kupitia nayo imeyalaani mauaji hayo ya Bi Benazir Bhutto ambaye chama chake cha PPP kina wafausi wengi zaidi nchini Pakistan.