1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bhutto anusurika katika shambulio la kutaka kumuuwa

Mohammed Abdulrahman19 Oktoba 2007

Watu wapatao 130 wameuwawa katika shambulio hilo la kujiripua kwa kujitoa mhanga dhidi ya Waziri mkuu huyo wa zamani wa Pakistan mjini Karachi.

https://p.dw.com/p/C77f
Watu wakiwasaidia majeruhi baada ya shambulio hilo la mabomu mjini Karachi
Watu wakiwasaidia majeruhi baada ya shambulio hilo la mabomu mjini KarachiPicha: AP

Shambulio hilo la mabomu lilifanywa wakati Bibi Benazir Bhutto akisindikizwa na umati mkubwa wa wafuasi wake waliojazana mitaani kumaki baada ya kuwasili jana mjini Karachi akitokea uhamishon,, akitokea London kupitia Dubai.

Kwa mujibu wa maafisa wa polisi zaidi ya watu 130 wameuwawa na duuru za hospitali zinasema karibu watu 400 wamejeruhiwa. Bibi Bhutto alisalimika akipata majeraha madogo na kukimbizwa nyumbani baada ya tukio hilo.

Mkuu wa polisi mjini Karachiv, Azhar Farooqi alisema bomu la kutupa kwa mkono lilirushwa katikati ya umati wa watu, na sekunde chache baadae mtu mmoja akajiripua .Waziri wa ndani Aftab Sherpo amesema kilikua ni kitendo cha kigaidi dhidi ya Bibi Bhutto na kimelengwa katika kuuhujumu utaratibu wa demokrasia nchini humo.

Kabla ya kurudi nyumbani Bhutto aliombwa na Rais Pervez Musharraf achelewesha safari yake kwa sababu ya usalama, lakini waziri mkuu huyo wa zamani akapuuza wito huo akisema hatowapigia magoti magaidi na anarudi bila ya hofu dhidi ya maisha yake.

Baada ya shambulio hilo Bibi Bhutto alikimbizwa nyumbani na mipango ya kuuhutubia wafuasi wake leo imefutwa. Polisi imesema kimegunduliwa kichwa cha mtu anayeshukiwa ndiye aliyejiripua na kwamba uchunguzi uchunguzi umeanza .

Akizungumzia suala la usalama kwa kiongozi huyo baada ya tukio hilo, mwenyekiti wa chama chake cha Pakistan Peoples-PPP Qassim Zia alisema,“Nafikiri sasa kwa kuwa hili limetokea kuna haja ya usalama kuimarishwa zaidi. Na kuhusu ratiba ya ziara zake hilo litaamuliwa na kamati kuu ya chama.”

Viongozi na nchi kadhaa duniani zimelani shambulio hilo, wakiwemo Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa, mawaziri wakuu wa Uingereza Gordon Brown na John Howard wa Australia ,Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon, na pia Umoja wa Ulaya

Marekani inayoingalia Pakistan kama mshirika wake muhimu katika vita dhidi ya ugaidi imelilaani shambulio hilo .Msemaji wa masuala ya usalama wa taifa katika Ikulu ya Marekani Gordon Johndroe alisema pamoja na hayo kuwa nchi yake inaomboleza kupotea kwa maisha ya waliouwawa.

Risala za kulaani shambulio hilo zimetolewa pia Indonesia amabayo binafsi imeshuhudia hujuma kadhaa za kigaidi, China iliotoa wito kwa Pakistan kudumisha umoja wa taifa, na jirani yake India iliosisitiza juu ya haja ya kuwepo kwa mshikamano zaidi kupambana na ugaidi.

Rais wa Pakistan Pervez Musharraf amelitaja shambulio hilo la kutaka kumuuwa Bibi Bhutto kuawa ni njama ya kuhujumu demokrasia, lakini mumewe bibi Bhutto, Asif Ali Zaradari alisema katika mahojiano na stesheni moja ya televisheni kwamba anashuku huenda kuna watu ndani ya serikali waliohusika, wakihofia watapoteza nyadhifa zao ikiwa bibi Bhutto atarudi madarakani.

Kwa wajkati huu mji wa Karachi na taifa la Pakistan kwa jumla limo katika hali ya mshutuko.