1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Besigye awekwa kwenye kizuizi cha nyumbani

19 Mei 2011

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Uganda, Dk. Kizza Bessigye, amewekwa katika kifungo cha nyumbani na serikali ya nchi hiyo, ambapo amezuiliwa kutotoka nje ya nyumba yake.

https://p.dw.com/p/11Jdx
Kizza Bessigye akizungumza na waandishi wa habari
Kizza Bessigye akizungumza na waandishi wa habariPicha: AP

Hatua hii inakuja muda mchache tu kabla ya kufanyika kwa maandamano ya kuipinga serikali yaliyopangwa hii leo (Alhamis 19 Mei 2011) mjini Kampala.

Msemaji wa polisi, Judith Nabakooba, amesema kuwa hatua hii inakusudiwa kuepusha ghasia. Wanaharakati wa upinzani wamesema, mapema leo hii polisi iliyazingira makaazi ya Bessigye huko Kasangati, kiasi cha kilomita 16 kaskazini mwa mji mkuu wa Kampala.

Tangu mwezi Aprili, Bessigye amekuwa akiongeza kampeni ya kutembea kwa miguu iliyopewa jina na "Walk-to-Work" kupinga mfumko wa bei za chakula na mafuta nchini humo, ambayo polisi wamekuwa wakiiazima kwa kutumia risasi za moto na mabomu ya kutoa machozi.

EU yaimwagia DRC mamilioni ya euro kufanya uchaguzi

New York:

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine AshtonPicha: dapd

Umoja wa Ulaya (EU) umekubali kuipa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) kiasi ya euro milioni 47.5 kusaidia mchakato wa uchaguzi unaopangwa kufanyika Novemba 28 mwaka huu.

Kwenye kikao cha jana cha Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, kilichofanyika mjini New York, Marekani, Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa DRC, Raymond Tshibanda, alisema serikali yake imepungukiwa na asilimia 40 ya fedha zinazohitajika kuandaa uchaguzi huo.

Mjumbe wa EU katika Umoja wa Mataifa, Pedro Seranno, aliuambia mkutano wa Baraza la Usalama kuwa serikali ya DRC imepiga hatua kubwa katika kuimarisha taasisi za demokrasia na inahitaji kuendelea kusaidiwa.

Fedha zitakazotolewa na EU zitatumika kununulia vifaa vya mawasiliano kwa ajili ya polisi na kusaidia tume ya waangalizi ya Umoja huo itakayotumwa DRC.

Mauaji mapya nchini Somalia

Mogadishu:

Makruti wa Jeshi la Somalia wakiwa mafunzoni nchini Uganda
Makruti wa Jeshi la Somalia wakiwa mafunzoni nchini UgandaPicha: AP

Watu wasiopungua 14 wameuwawa kufuatia mapambano makali kati ya wapiganaji wa Kiislamu na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika (AMISOM) katika soko la Bakara mjini Mogadishu, Somalia.

Mkuu wa huduma za dharura mjini humo, Ali Muse, amesema makombora yaliyovurumishwa kwenye soko hilo, yaliwajeruhi pia raia wengine zaidi ya 60.

Naye msemaji wa AMISOM, Paddy Ankunda, alisema Jumatatu wiki hii kwamba wanajeshi wa Uganda na Burundi walioko Mogadishu, waliazisha kampeni mpya mapema mwezi huu kuyalenga maeneo yanayodhibitiwa na kundi la Al-Shabbab. Ankunda alisema kwa sasa AMISOM inadhibiti asilimia 60 ya mji mkuu wa Mogadishu.

Ushelisheli waingia uchaguzini

Victoria:

Zoezi la uchaguzi
Zoezi la uchaguziPicha: DW

Wapiga kura katika visiwa cha Ushelisheli wameanza kupiga kura hii leo kumchagua kiongozi mpya, huku rais wa sasa, James Michel, akipewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo uliotawaliwa na mjadala kuhusu mageuzi ya kiuchumi. Upigaji kura umepangwa kufanyika kwa siku tatu.

Mbali na Rais Michel, ambaye amekuwa akitawala tangu mwaka 2004, kuna wagombea wengine watatu wanaowania urais. Mpinzani mkuu wa kiongozi huyo ni Wavel Ramkalawan wa chama cha kizalendo cha Ushelishli, SNP, ambaye anagombea kwa mara ya nne. Wengine ni Ralph Volcer wa chama kipya cha kidemokrasia, NDP, na Philippe Boulle, ambaye ni mgombea wa kujitegemea.

Wapigaji kura 70,000 wamejiandikisha kupiga kura na baadhi watalazimika kusubiri hadi kesho Ijumaa au Jumamosi ili waweze kupiga kura. Licha ya idadi ndogo ya wakaazi katika visiwa vidogo vya Ushelisheli, maafisa wa tume ya uchaguzi wamekuwa wakisafirisha vifaa vya kupigia kura kutumia boti na ndege.

Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa wiki ijayo.

Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutembelea Afrika

Addis Ababa:

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Baraza Kuu la Umoja wa MataifaPicha: AP

Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa utafanya mazungumzo na serikali za Ethiopia, Sudan na Kenya kuhusu maswala ya amani na usalama katika kanda hiyo.

Umoja wa Mataifa umesema kwanza ujumbe huo utafanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi, mjini Addis Ababa hapo kesho. Kisha maafisa hao wataelekea Sudan, ambako wanapanga kukutana na viongozi wa huko kuzungumzia kura ya maoni iliyokubalia kujitenga kwa Sudan Kusini. Pia utakutana na vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani nchini humo.

Mjini Nairobi, ujumbe huo utajadili maswala yanayoihusu Somalia na pia kukutana na maafisa wakuu wa serikali ya Kenya. Ujumbe huo utakamilisha ziara yao tarehe 26 mwezi huu na kurejea mjini New York.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, siku ya Jumamosi anatarajiwa kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais mpya wa Cote d' Ivoire, Alassane Ouattara.

Burundi kuunda Baraza la Haki za Binaadamu

Bujumbura:

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi
Rais Pierre Nkurunziza wa BurundiPicha: picture alliance / dpa

Bunge la Burundi leo linatarajiwa kujadili na kuidhinisha wajumbe saba wa Baraza la Haki za Binaadamu, litakalokuwa na jukumu la kufuatilia kwa karibu hali ya haki za binaadamu nchini humo.

Kikao cha leo kinafanyika kufuatia ahadi ya Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, hapo jana kwamba watu waliohusika kufanya machafuko ya kisiasa nchini humo watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria siku chache zijazo kujibu mashtaka.

Rais huyo aidha alisema atahakikisha haki imetendeka na hakuna anayepaswa kudhani anaweza kuukwepa mkono wa sheria au kukimbilia hifadhi nchini Tanzania au katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Mwandishi: Bruce Amani

Mhariri: Othman Miraji