Berlusconi kufikishwa mahakamani | Masuala ya Jamii | DW | 16.02.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Berlusconi kufikishwa mahakamani

Jaji wa mahakama nchini Italia ameamuru kuwa waziri mkuu wa Italia Silvio Berlusconi afikishwe mahakamani mwezi Aprili, akikabiliwa na mashtaka ya kumpa fedha msichana mdogo kwa nia ya kufanya nae ngono

default

Waziri mkuu wa Italia Silvio Berlusconi

Jaji wa mahakama nchini Italia ameamuru jana kuwa waziri mkuu wa Italia Silvio Berlusconi afikishwe mahakamani mwezi Aprili , akikabiliwa na mashtaka , kwamba alimpa fedha msichana wa umri wa miaka 17 kwa nia ya kufanya nae ngono na kutumia wadhifa wake kumtoa msichana huyo kutoka mikononi mwa polisi.

Jaji Cristina Di Censo amepanga kesi hiyo kusikilizwa kwa mara ya kwanza hapo Aprili 6 , katika hatua ambayo inaleta madai ya siku nyingi ya kashfa katika maisha ya kibinafsi ya kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 74 usoni, na kuchafua nafasi yake madarakani.

Kufuatia tangazo hilo, kambi ya waziri mkuu huyo , ilidai kuwa Berlusconi alikuwa mhanga wa kumchafulia jina , inayofanywa na wapinzani wake kisiasa.

Wakili wake amesema, kuwa hatukutarajia kitu kingine zaidi ya hiki.

Berlusconi , ambaye vituko vyake vya masuala ya chumbani , vimezusha maandamano ya nchi nzima yaliyofanywa na wanawake wa nchi hiyo mwishoni mwa juma , kesi yake itasikilizwa na majaji watatu wanawake, na hali hiyo imesababisha gazeti moja maarufu lijulikanalo kama , Familiglia Cristiana kudokeza kuwa waziri mkuu sasa amepata mbabe wake.

Italien Proteste gegen Berlusconi

Wanawake wakiandamana katika mitaa ya miji ya Italia

Wanasiasa wa upinzani wanadai Berlusconi ajiuzulu kutokana na kitendo hicho cha kufanya mapenzi na msichana mwenye umri mdogo na pia kutumia madarakani yake kinyume na utaratibu. Mbunge wa chama cha upinzani cha Kiliberali nchini Italia, Marco Perduca amesema kuwa mahakama nchini humo imechukua hatua za haraka kuisiliza kesi hii, kwa kuwa kesi za jinai na za kihalifu huchukua wastani wa miaka sita hadi saba nchini humo. Lakini hilo si muhimu, muhimu ni madai yenyewe.

Nadhani madai ya ukahaba si muhimu sana hapa, lakini muhimu ni madai ya kutumia vibaya madaraka yake. Ni lazima ifahamike kuwa Berlusconi , licha ya kuwa ni rais wa baraza la mawaziri, lakini pia ni mbunge , na ana kinga ya kutoshtakiwa, kwa hiyo lazima tufahamu ,ni hatua gani hapo baadaye zinaweza kuchukuliwa kabla ya kufikishwa mahakamani Aprili 6.

Berlusconi anakabiliwa na hukumu ya kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela iwapo atapatikana na hatia ya kumpa fedha mtoto mdogo kwa ajili ya ngono, na pia kutumia madaraka yake kuwalazimisha polisi kumwachia msichana huyo Ruby , baada ya kukamatwa kwa madai ya wizi na kumkabidhi msichana huyo kwa msichana mwingine, Nicole Minetti.

Lakini mwanasheria mmoja ambaye anahusika kwa karibu na kesi hiyo , amesema kuwa upande wa utetezi unaweza kujaribu kuonyesha wasi wasi wa uwezo wa mahakama ya mjini Milan kusikiliza kesi hiyo. Berlusconi anaweza pia kuitisha kura bungeni kuimarisha nafasi yake , na kudai kuwa kuwapo kwake madarakani kunamzuwia kuhudhuria kesi hiyo.

Hata kama atapatikana na hatia na kuhukumiwa, waziri mkuu huyo hafikiriwi kuwa atatumikia kifungo chake jela kwa kuwa muongozo wa hukumu nchini Italia , unakipengee cha huruma kwa watu waliofikia umri wa miaka ya 70, na Berlusconi ana umri wa miaka 74.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 • Tarehe 16.02.2011
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/10HmQ
 • Tarehe 16.02.2011
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/10HmQ

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com