1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Berlusconi ashinda Itali

15 Aprili 2008

Silvio Berlusconi ameshinda uchaguzi wa jana wa bunge na kwa mara ya 3 anakuwa waziri mkuu wa Itali.

https://p.dw.com/p/DiA5
BerlusconiPicha: AP

Silvio Berlusconi-tajiri mkubwa wa vyombo vya habari nchini Itali,ameshinda uchaguzi wa jana wa Bunge nchini Itali na kwa mara ya tatu anakua waziri mkuu.Mpinzani wake Veltroni hakukawia jana kumpongeza kwa ushindi wake huo.

Muda mfupi baada ya saa 3 usiku saa za Afrika mashariki hapo jana ,mtetezi wa chama cha Democratic Party, Walter Veltroni aliungama kushindwa na akamnyoshea mkono wa pongezi Silvio Berlusconi:

"Kama ilivyo desturi ya demokrasia katika nchi za magharibi na kwa muujibu nionavyo mimi ni barabara, nimempigia simu Kiongozi wa chama cha "Umma Huru" na kumpongeza kwa ushindi wake .Pia nilimtakia mafanikio kwa kazi yake ,jambo ambalo wakati huu kwa kila mtaliana anaeitakia mema nchi yake apaswa kufanya."

Makisio ya kwanza kabisa baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura ,yalibainisha watetezi hao wawili Berlusconi na Veltroni wako bega kwa bega.Yalibainisha kuja kuundfwa kwa serikali ya muungano kati ya kundi la Berlusconi na chama cha Democratic party cha mrengo wa shoto kikiongozwa na Veltroni.

Katika makisio yote yaliofuata,Berlusconi alianza kutia fora usoni na mwishoe ikadhihirika dhahiri-shahiri kwamba Bw.Berlusconi ameshinda wazi kwa kujipatia viti vingi Bungeni. Amejipatia 46% ya kura katika BARAZA LA SENAT wakati Veltroni 38% tu.Hata katika Bunge la pili,Berlusconi amejipatia 45% kwa 38% za Veltroni.

Kutokana na uchaguzi wa jana vyama vidogo vidogo ndivyo vilivyopatwa na maafa.

Kwa msangao wa wengi ushirika wa vyama vya mrengo wa shoto-wakoministi na walinzi wa mazingira ,ulikwama kwa kutovuka kizingiti cha 4%.

Pia vikundi vya mrengo wa kulia vya wafashisti-mambo-leo na vyenginevyo vilianguka kwa kutovuka kizingiti hicho cha 4%.

Schifani, mshirika wa chanda na pete wa Silvio Berlusconi,ameueleza ushindi huo kuwa ni wa kihistoria unaofungua ukurasa mpya kwa Itali.

Wakati wa vyama vidogo vidogo nchini Itali umemalizika.

Schifani asema:

"Nahisi mfumo wa vyama viwili vikuu vinavyoshindana umeshaimarika na ndicho watakacho wataliana.Sasa ni jukumu la serikali na Upinzani, kutimiza hamu ya wataliana kuendeleza mfumo huu.

Hii maana yake , sisi na Upinzani tushirikiane kuamua jinsi gani kuzigeuza kanuni zinavo stahiki kufuatwa nchini."

Ishara ya kwanza ya kutaka ushirikiano ambayo itabadili mtindo wa kuendesha siasa nchini Itali imetoka kwa kambi ya Berlusconi.Badala ya mtindo wa zamani wa kupeana changamoto na kukaripiana ,Schifani na wajumbe wengine wa ushirika wao wa mrengo wa kulia walipendekeza tangu usiku wa ja a wa uchaguzi mazungumzo na kambi ya mrengo wa kushoto.

Kwa muujibu wa matokeo ya sasa ,Silvio berlusconi na muungano wake wa kulia aweza kutawala katika mabaraza yote 2 bila ya wasi wasi wowote.Chama cha Lega Nord kimeimarika zaidi kufuatia uchaguzi wa jana na kinadai makuu.Kinadai mamlaka zaidi ya kujiendeshea mambo yake eneo la kaskazini la Itali ambalo ndilo lililoendelea kiuchumi na huenda ikatoa changamoto kali kwa waziri-mkuu mpya na wa zamani Silvio Berlusconi.