1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN:Maonyesho ya ITB yafunguliwa rasmi

7 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCLU

Maonyesho ya bishara ya Utalii ya kimataifa yanafunguliwa rasmi hii leo mjini Berlin na kuendelea hadi tarehe 11 mwezi huu.Maonyesho hayo yanahusisha makampuni alfu 11 kutoka mataifa 184 huku India ikiwa nchi shirika.

Katika ufunguzi rasmi nchi ya India ilionyesha utamaduni wake uliohudhuriwa na Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Michael Glos na Waziri wa Utalii wa India Ambika Soni.Wito wa kuongeza kodi katika safari za ndege ili kupambana na ongezeko la viwango vya joto ulimwenguni ulihakirishwa na Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Michael Glos.

Kulingana na Bwana Glos hatua ya kulipisha kodi mafuta ya ndege huenda ikaathiri nafasi za kazi katika sekta hiyo.hatua hiyo inapigiwa debe na wanamazingira wanaoshikilia kwamba hilo litapunguza idadi ya safari za ndege.Aliongeza kuwa kutoza taifa moja ada hiyo na kuacha mengine si haki.

Maonyesho hayo yanafanyika wakati ishara za ongezeko la viwango vya joto ulimwenguni zinadhihirika kote ulimwenguni hasa katika maeneo ya thuluji ambako inayeyuka huku kina cha maji kikiongezeka katika visiwa vya Bara Hindi.

Waandaji wa maonyesho hayo wanawaomba wataalam kuhudhuria ili kuzungumzia mustakabal wa usafiri.

Kwa mara ya kwanza maonyesho ya ITB yanajumuisha banda la wauzaji nyumba ili kuwavutia wateja matajiri wasioweza kuzuru maeneo ya mapumziko.