1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN:Baraza la mawaziri labadili sheria ya uhamiaji

28 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCEm

Baraza la Mawaziri nchini Ujerumani wameidhinisha mabadiliko kwenye sheria ya uhamiaji yatakayowezesha takriban watu laki moja themanini wanaotafuta hifadhi kupewa ruhusa ya kuwa wakazi.Watu hao walinyimwa hifadhi.Kulingana na sheria hiyo mpya mtu yoyote ambaye amekuwa akiishi Ujerumani kwa yapata miaka sita na ana ujuzi wa lugha ya Kijerumani anaweza kuomba ruhusa ya kuwa mkazi wa muda ifikapo mwezi Julai.Sheria hiyo inawawezesha walionyimwa hifadhi na hawawezi kurudishwa nchini mwao kwasababu za kiusalama.

Watu watakaofanikiwa wanaruhusiwa kuendelea kubaki nchini hata baada ya mwaka 2009 iwapo watapata nafasi za kazi.Sheria hiyo kwa upande mwingine haijumuishi raia takriban milioni moja wa kigeni wanaoishi Ujerumani kinyume na sheria na hawajaomba hifadhi.

Kwa mujibu wa Waziri wa mambo ya ndani Wolfgang Schaeuble sheria hiyo mpya inalenga kuwianisha Ujerumani na sheria za kuomba hifadhi za Umoja wa Ulaya vilevile kuwaeleza wakazi kuwa raia wa kigeni hawataipa mzigo mzito idara ya malipo ya umma.

Sheria hiyo inasubiri kuidhinishwa na bunge lililo na idadi kubwa ya wanachama wa chama tawala.