1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benjamin kuzungumzia sera yake kuu ya nje

Amina Mjahid
5 Machi 2018

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu atakutana na rais wa Marekani Donald Trump hali ambayo itatowa nafasi ya kumuondoa kwa muda katika uchunguzi wa kashfa ya ufisadi inayozidi kumuandamana nchini mwake

https://p.dw.com/p/2tit7
USA Israel Trump und Netanjahu Israel Museum in Jerusalem
Picha: Reuters/R. Zvulun

Viongozi hao wawili Benjamin Netanyahu wa Israel na Donald Trump wa Marekani wanatarajiwa kuwa na msimamo wa pamoja dhidi ya uchokozi unaofanywa na Iran hasa nchini Syria na kutoa wito wa kuboreshwa kwa mpango uliyoafikiwa wa Nyuklia kati ya taifa hilo na mataifa sita yaliyo na nguvu duniani. Trump ametishia kuyavunja makubaliano hayo.

Katika mkutano wao utakaofanyika kwenye ikulu ya White house, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anatarajiwa kumpongeza Trump kwa hatua yake ya kuitambua Jerusalem kama mji Mkuu wa Israel na kuhamisha ubalozi wa Marekani katika eneo hilo.

"Natarajia kuzungumza naye kuhusu masuala mengi lakini kwanza ni juu ya Iran, uchokozi wake, matarajio yake ya nyuklia na hatua yake pia ya kichokozi katika eneo la Mashariki ya kati na mipaka yetu. Nadhani hatua ya kuzuwia uchokozi huu ni lengo letu la pamoja na la mataifa mengine katika eneo,”alisema Benjamin Netanyahu.

Hata hivyo ziara hii ya Nentanyahu nchini Marekani inakuja wakati ambapo waziri mkuu huyo  anapitia wakati mgumu nyumbani, wakati Mwanasheria Mkuu akifikiria iwapo achukue hatua kutokana na mapendekezo ya polisi kwamba amfungulie mashtaka dhidi ya rushwa na mashitaka mengine.

USA Israel | Benjamin Netanjahu bei Donald Trump in Washington
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Getty Images/A. Wong

Netanyahu na mkewe Sara, waliwasili mjini Washington hapo jana siku mbili baada ya kuhojiwa kwa saa kadhaa na polisi nchini Israel juu ya tuhuma za  rushwa zinazofungamanishwa na kampuni ya simu ya telecom. 

Mkutano wake na Trump na hotuba yake aliyoitoa katika mkutano wa kamati ya masuala ya Umma ya Marekani ambayo ina jukumu la kulinda maslahi ya Israel (AIPAC) inammpa nafasi Netanyahu kuangazia wasiwasi katika sera yake ya kigeni pamoja na mafanikio.

Kikubwa katika orodha yake hii ni Marekani kuutambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel, hatua ambayo iliwakasirisha wapalestina na kukosolewa Kimataifa lakini hilo limempa sifa Netanyahu nchini Israel. Awali rais wa Guatemala Jimmy

Morales alitangaza mipango ya nchi yake ya kuuhamisha ubalozi wake mjini Jerusalem.

Aidha Mchakato wa mazungumzo ya amani au upatanishi kati ya Israel na palestina umesimama tangu rais Trump kutangaza hatua hiyo ya kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel lakini maafisa wa Ikulu ya Marekani wanasisitiza kwamba watawasilisha mpango wa amani hivi karibuni.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa 

Mhariri: Yusuf Saumu