1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIRUT: Merkel ziarani Lebanon

2 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCDB

Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel ameanza mazungumzo na viongozi wa Lebanon mjini Beirut hii leo. Awamu ya kwanza ya mazungumzo itatuwama juu ya uhusiano baina ya Lebanon na Ujerumani.

Msemaji wa serikali ya Lebanon mjini Beirut amesema waziri mkuu Fouad Siniora atamtarifu kansela Merkel juu ya mgogoro wa kisiasa nchini Lebanon. Katika awamu ya pili ya mazungumzo yake kansela Angela Merkel atajadili hatua ya serikali yake kuendelea kuunga mkono uhuru wa Lebanon. Atazungumzia juu ya wanajeshi wa Ujerumani katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL.

Kiongozi huyo aliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mjini Beirut chini ya ulinzi mkali na kulakiwa na mwenyeji wake waziri mkuu, Fouad Siniora, kabla kupelekwa katika ikulu.

Ghinwa Jaloul, kiongozi katika idara ya serikali ya Lebanon ameitaka Ujerumani iisaidie Lebanon.

´Kwa hiyo ningependa kuwaona Wajerumani wakiisaidia Lebanon na kuizuia Israel au kuchukua hatua za kuizuia Israel kuishambulia Lebanon. Tungependa rafiki yatu atusaidie kuilinda Lebanon. Lebanon haiwezi kukabiliana na shambulio lengine wakati huu ikijenga upya miundombinu yake. Sisi ni taifa la amani, tunataka amani. Kwa hiyo naamini msaada huu ni muhimu.´

Kansela Merkel anatarajiwa kukutana na spika wa bunge la Lebanon, Nabih Berri kabla kuwa na mazungumzo na waziri mkuu Fouad Siniora baadaye leo.