1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIRUT : Maandamano kushinikiza kun’gatuka kwa serikali

10 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCkb

Katika mji mkuu wa Lebanon Beirut mamia kwa maelfu ya wafuasi wa upinzani unaongozwa na kundi lenye kuiunga mkono Syria la Hezbollah wanatarajiwa kufanya maandamano makubwa leo hii yenye lengo la kuendelea kushinikiza kun’gatuka kwa serikali ya nchi hiyo inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi.

Wafuasi wa upinzani wamekuwa wakipiga kambi katikati ya jiji la Beirut tokea Desemba Mosi wakiapa kwamba hawatosalimu amri hadi hapo Waziri Mkuu Fouad Siniora atakapokubali madai yao ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Upinzani unasema kwamba serikali iliopo hivi sasa haiwakilishi tena wananchi wa Lebanon baada ya mawaziri sita wanaoiunga mkono Syria kujiuzulu mwezi uliopita.Washirika wa Siniora wanasema inachotaka Hezbollah ni kuvuruga tu mipango ya kuunda mahkama ya kimataifa kuwashtaki watuhumiwa wa mauaji ya Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik al Hariri hapo mwaka 2005 ambayo Walebanon wengi wanailaumu Syria kwa kuwa na mkono wake.

Rais Emile Lahoud wa Lebanon anayeiunga mkono Syria amekataa rasmi mipango ya kuundwa kwa mahkama hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.