1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIJING: Rice njiani kwenda Moscow

21 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD0U

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Bi Condoleezza Rice ameondoka mjini Beijing China kwenda Moscow Urusi kuendeleza mazungumzo juu ya Korea Kaskazini. Bi Rice anatarajiwa kukutana na rais wa Urusi, Vladamir Putin mjini Moscow.

Safari yake ya kwenda Urusi inafanyika baada ya utawala wa Korea Kaskazini kutangaza hautafanya jaribio lengine la zana za kinyuklia. Shirika la habari la Korea Kusini, Yonhap, limeripoti kwamba Korea Kaskazini haina nia ya kufanya majaribio zaidi ya silaha zake za kinyuklia.

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong- il, amenukuliwa akimwambia mjumbe wa China, Tang Jiaxuan, kuhusu uamuzi wake wa kusimamisha majaribio ya kinyuklia wakati wa mazungumzo yao ya juzi Alhamisi.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Japan, imesema haiwezi kuthibitisha wala kukanusha ripoti hiyo. Akiwa mjini Beijing Condoleezza Rice aliihimiza China itekeleze kikamilifu na kwa haraka vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini kufuatia jaribio lake la kinyuklia lililofanywa Oktoba 9.

Beijing kilikuwa kituo cha mwisho cha waziri Rice katika zaira yake barani Asia iliyolenga kutafuta uungwaji mkono wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini.