1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIJING: Merkel akutana na waandishi wa habari wa China

28 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBV6

Kansela wa Ujerumani, Bi Angela Merkel, leo amekutana na waandishi wanne wa habari walio wakosoaji wakubwa wa sera za serikali ya China.

Mazungumzo ya kansela Merkel na waandishi hao wanaojulikana kwa kuikosoa serikali katika maswala ya mageuzi ya kisiasa na ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari ni sehemu ya mpango rasmi wa kuangazia umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari nchini China.

Kiongozi huyo pia amesema hatua ya Beijing kuandaa michezo ya Olimpik mwakani itatoa mwanya kuchunguza mwenendo wa nchi hiyo kuhusiana na swala la haki za binadamu katika miaka iliyopita.

Aidha Bi Merkel amesema ulimwengu unasubiri kuona jinsi China itakavyoruhusu uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari wakati wa michezo hiyo ya Olimpik.

Angela Merkel pia ameishutumu China kwa kutengeneza motokaa zinazoigiza miundo ya motokaa za Ujerumani, ambazo zitaonyeshwa kwenye maonyesho ya magari mjini Frankfurt hapa Ujerumani mwezi ujao.

Kiongozi huyo ameyasema hayo hii leo wakati alipotoa hotuba katika chuo cha sayansi ya jamii mjini Beijing.

Kansela Merkel ametoa matamashi hayo siku moja baada ya kukutana na rais wa China hiyo, Hu Jintao na waziri mkuu Wen Jiabao, ambapo alizungumzia maswala ya haki za binadamu, biashara, ulinzi wa mazingira na tabia ya China kuiba haki miliki.

´Hiyo ina maana tunalazimika kwa haraka kuleta teknolojia mpya na China inajua kwamba katika siku za usoni itakuwa na jukumu kubwa. Lakini naelewa pia kwamba maendeleo ya kiuchumi lazima yafikiwe.´

Ziara ya kansela Merkel nchini China, imeingia siku yake ya pili hii leo.