1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yazidi kujichimbia kileleni

24 Februari 2014

Bundesliga, Bayern yaendelea kupeta , Dortmund yaangukia pua, wakati Hamburg ikionesha matumaini ya kubaki katika daraja la kwanza, Champions League kuunguruma tena wiki hii.

https://p.dw.com/p/1BEbA
Fußball Bundesliga Hannover 96 vs. FC Bayern München
Wachezaji wa Bayern wakirejea kutoka katika operesheni ya kuweka mpira wavuni dhidi ya HannoverPicha: AFP/Getty Images

Ilikuwa ni wiki ya matumaini kwa vigogo wa soka timu kongwe ya Hamburg SV nchini Ujerumani , baada ya kufufua matumaini yao kwa kuikandika Borussia Dortmund kwa mabao 3-0 katika mchezo wao wa kwanza chini ya kocha mpya Mirko Slomka.

Kocha huyo ambaye ni wa tatu msimu huu ameonesha kuwa kikosi hicho cha klabu kongwe nchini Ujerumani ya Hamburg ina uwezo wa kubakia katika daraja ya juu, kuliko ilivyoonekana wiki iliyopita baada ya kupata kipigo cha sita mfululizo dhidi ya Eintracht Braunschweig.

Fußball Bundesliga Hamburger SV vs. Borussia Dortmund
Kocha Mirko Slomka akifurahia kazi ya kikosi chake dhidi ya DortmundPicha: Getty Images

Mwanzoni mwa mchezo huo Dortmund ilionekana kuudhibiti mchezo, lakini Hamburg waliimarisha ulinzi na Dirtmund hawakuweza kuipasua ngome ya timu hiyo.

Kwa ushindi huo muhimu kwa Hamburg , timu hiyo imejitoa kutoka katika eneo la hatari ya kushuka daraja , lakini Dortmund ilishindwa kuchupa na kuchukua nafasi ya pili na badala yake ilibakia katika nafasi ya tatu, licha ya Bayer Leverkusen iliyoko nafasi ya pili ya msimamo wa ligi kupata kipigo nayo cha mabao 3-1 dhidi ya Wolfsburg.

Viongozi wa ligi hiyo hata hivyo Bayern Munich imeendelea kuliacha kundi la timu nyingine 17 na kujiweka peke yake juu bila mpizani wa karibu. Bayern ilipata ushindi tena wa mabao 4-0 dhidi ya Hannover 96 ikiwa ni ushindi wa 20 mfululizo msimu huu na hakuna dalili kwamba kuna timu katika bundesliga inayoweza kupimana kifua na Bayern Msimu huu.

Fußball Bundesliga Hamburger SV - Borussia Dortmund
Bao likitinga katika nyavu za DortmundPicha: picture-alliance/dpa

Na katika ligi nyingine katika bara la Ulaya, Atletico Madrid imeshindwa kuchukua fursa ya kujiunga na Real Madrid katika nafasi ya juu ya msimamo wa ligi ya Uhispania, La Liga wakati walipokubali kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Osasuna jana Jumapili(23.02.2014).

Fußball Bundesliga Hamburger SV - Borussia Dortmund
Wachezaji wa Hamburg wakipongezana kwa kazi nzuri dhidi ya DortmundPicha: picture-alliance/dpa

Real Madrid imejisogeza points tatu zaidi juu kutoka washindani wake wa karibu , Barcelona na Atletico Madrid, ambapo timu hizo zote zina points 60 wakati Real Madrid ikiwa na points 63.

Mabingwa Barcelona walipokea kipigo cha mabao 3-1 siku ya Jumamosi dhidi ya Real Sociedad, wakati uamuzi wa kocha Gerardo Martino wa kuwapumzisha wachezaji muhimu kadha uliposababisha maafa.

Premier League

Huko nchini Uingereza, katika Premier League, viongozi wa ligi hiyo kwa sasa Chelsea wameendelea kuongoza kwa point moja zaidi ambapo inafuatiliwa kwa karibu na Arsenal London na points tatu mbele ya Manchester City baada ya goli la nahodha John Terry kuizamisha Everton.

John Terry mit Kapitänsbinde
Nahodha wa Chelsea , John TerryPicha: dapd

Magoli saba yalitinga nyavuni jana katika mchezo wa kuvutia kati ya Liverpool na Swansea City , ambapo kikosi cha kocha Brendan Rodgers kilipata ushindi wa mabao 4-3 na kujiweka katika nafasi ya nne katika Premier League.

Borussia Dortmund yasua sua:

Borussia Dortmund inachechemea na inaelekea nchini Urusi kupambana na Zenit Saint Petersburg katika pambano la Champions League kesho Jumanne katika mchezo wa kwanza wa timu 16 zilizosalia katika kinyang'anyiro hicho ikifuatwa nyuma na matatizo ya majeruhi katika kikosi chake.

Timu hiyo iliyofikia fainali ya Champions League msimu uliopita itakosa huduma ya mchezaji wake wa kati Sven Bender ambaye ameumia na atapumzika kwa wiki 10, pamoja na mlinzi Mats Hummels.

Hali kadhalika Manchester United ambayo inasua sua pia katika ligi ya Uingereza itajaribu kuonesha kuwa inaanza kupata nafuu hapo kesho katika mchezo mwingine dhidi ya Olympiakos Piraeus ya Ugiriki.

Bundesliga 15. Spieltag, Borussia Dortmund - Bayer 04 Leverkusen
Sven Bender akitolewa nje akiwa majeruhiPicha: picture-alliance/dpa

Mabingwa hao wa Ugiriki ambao wamefikia hatua hii kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka minne, watahitaji kufanya maajabu ya kihistoria kuwashinda United baada ya kushindwa mara nne timu hizo zilipokumbana hapo nyuma.

Siku ya Jumatano ni zamu ya timu nyingine ya Ujerumani miongoni mwa timu nne zilizoingia katika awamu hii, Schalke 04 ikiikaribisha Real Madrid, na pia Galatasaray Instanbul ya Uturuki itakuwa wenyeji wa Chelsea kutoka mjini London.

Kombe la mataifa ya Ulaya UEFA 2016

Kwa upande wa kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani kitaanza kusaka nafasi ya kushiriki katika fainali za kombe la mataifa ya Ulaya mwaka 2016 dhidi ya Scotland. Upangaji wa makundi ulifanywa jana Jumapili mjini Nice , unaonesha kuwa kikosi hicho cha kocha Joachim Loew kitakumbana na Poland Oktoba 14 na kisha kitakutana na Ireland nyumbani baadaye katika kundi D.

Timu nyingine katika kundi hilo ni kikosi kipya katika soka la Ulaya cha jimbo la Gibralter. Gibralter ilikubaliwa kuwa mwanachama mpya wa UEFA mwaka jana na ilibidi kubadilishwa kundi baada ya kupangwa katika kundi moja la C na Uhispania, nchi ambayo inadai kuwa jimbo hilo ni lake. Hatua hiyo inaziweka Uhispania na Uingereza katika mvutano mkubwa, ambapo nayo Uingereza inadai kuwa Gibralter ni jimbo lake.

Mchezo wa mwisho wa kufuzu kwa ajili ya fainali hizo zitakazofanyika nchini Ufaransa kuanzia Juni 10 hadi Julai 10 mwaka 2016 utakuwa Oktoba 8 , 2015 dhidi ya Irland na Oktober 11, 2015 dhidi ya Georgia. Kocha Joachim Loew alikuwa na haya ya kusema.

DFB Joachim Löw Trainer
Kocha wa Ujerumani Joachim LoewPicha: Martin Rose/Bongarts/Getty Images

"Nafikiri , tukiangalia kwa upande wa kimichezo, ni hali ya kuvutia, lakini pia inagusa hali halisi, pamoja na shauku. Kwa Ireland na Scotland, hapa tunafahamu la kufanya, kwa kuwa tunajua jinsi timu hizi zinavyocheza. Kwa hiyo nafikiri ni kundi la kuvutia kwetu. Tumekuwa kila mara na kiwango, cha kuweza kushinda katika makundi na pia kufuzu kucheza katika fainali."

Kwa upande wa Gibralter nchi ambayo ina wakaazi 30,000 ni kibarua kigumu sana kuweza kufuzu kwa ajili ya fainali hizi zitakazokuwa na washiriki 24 mara hii nchini Ufaransa, lakini Gibralter ina shauku kushiriki katika zoezi hilo.

Michezo ya olimpiki ya majira ya baridi mjini Sochi.

Michezo hiyo ya majira ya baridi ilifikia mwisho jana Jumapili ambapo wenyeji Urusi imejinyakulia medali nyingi zaidi na Canada ikanyakua taji la mpira ya magongo katika barafu kwa wanaume, lakini taarifa kwamba wachezaji wawili zaidi wamegundulika kutumia madawa yaliyopigwa marufuku ya kuongeza nguvu misuli zimeleta hali ya kufifia kwa mwanga wa mashindano hayo.

Canada ilijinyakulia ubingwa wa mpira wa magongo kwa kuiangusha Sweden kwa mabao 3-0 na kutetea ubingwa wao huo kwa wanaume, lakini ushindi mara mbili kwa Urusi umeihakikishia nchi hiyo kupata medali 13 za dhahabu dhidi ya 11 za Norway.

Madhila ya Sweden yaliongezwa na taarifa kuwa mshambuliaji wao Nicklas Backstrom amegundilika kuwa anatumia madawa ya kuongeza nguvu misuli , Doping. Maafisa wa timu hiyo wameilalamikia kamati ya kimataifa ya Olimpiki , IOC kwasababu walifahamishwa saa mbili tu kabla ya mchezo huo. Hata hivyo rais wa IOC Thomas Bach amesema kuwa wenyeji Urusi wamedhihirisha kuwa wakosoaji wao hawakuwa sahihi.

Kwa upande wa kikosi cha Ujerumani katika michezo hiyo mambo hayakuwa kama yalivyotarajiwa. Hali ya mambo anasema kiongozi wa kikosi hicho Michael Vesper haikuwa nzuri.

"Lengo letu halikutimia. Tumekuwa na matokeo mazuri kabisa katika wiki moja na nusu ya mwanzo, ambapo tulionesha ubora wetu kwa mataifa. Na baada ya hapo mambo hayakwenda vizuri."

Thomas Bach (WADA-Konferenz in Johannesburg)
Rais wa IOC , Thomas BachPicha: picture alliance/AP Photo

Hadi wakati huo wa kuporomoka , Evi Sachenbacher-Stehle mchezaji wa mbio za kwenye barafu na kulenga shabaha, alionekana tu kwamba madawa hayo yalionekana kuwa ni virutubisho katika chakula. Na kamati ya kimataifa ya olimpiki ilikubali matokeo ya mchezaji huyo katika michezo ya Sochi. Lakini siku ya Jumamosi mchezaji huyo alibidi kuondolewa kutoka katika kikosi cha Ujerumani. Waziri wa sheria wa Ujerumani Heiko Maas akizungumzia kuhusu hali hiyo amesema.

"Tunataka , kwamba hapo katika siku za usoni yeyoyte ambaye atapatikana na hatia kama hiyo ya doping, ama hata yeyote ambaye atapatikana na madawa kama hayo na pia kuuza , ataadhibiwa. Na kufungwa hadi miaka mitano jela."

Hiyo ndio hali iliyokuwa katika kambi ya kikosi cha timu ya Ujerumani katika olimpiki ya majira ya baridi ya mjini Sochi. Na hadi hapo ndio sina budi kusema tumefikia mwisho wa kuwaletea habari hizi za michezo kwa leo jina langu ni Sekione Kitojo, hadi mara nyingine kwaherini.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / afpe / rtre

Mhariri: Yusuf , Saumu