1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern ukingoni mwa kutawazwa mabingwa

Admin.WagnerD13 Aprili 2015

Bayern Munich iko karibu na kusajili ubingwa wake wa tatu katika ligi ya Ujerumani Bundesliga, Stuttgart yazinduka, yapata ushindi muhimu na kujitoa kutoka nafasi ya mkiani katika Bundesliga

https://p.dw.com/p/1F7D9
Fussball Bundesliga FC Bayern München gegen Eintracht Frankfurt
Kikosi cha Bayern Munich kinachotamba nchini UjerumaniPicha: Lennart Preiss/Bongarts/Getty Images

Bundesliga. Bayern Munich imefanikiwa kujisogeza karibu na ubingwa wake wa tatu mfululizo msimu huu baada licha ya timu zote nne zilizoko juu ya msimamo wa ligi kushinda michezo yao , lakini Bayern inabakia pointi 10 mbele ya timu zinazofuatia, wakati imebakia michezo sita kabla ya ligi kumalizika.

Bayern iliishinda Eintracht Frankfurt kwa mabao 3-0 ambapo mabao mawili yaliwekwa wavuni na Robert Lewandowski. Na anasema hiyo ndio kazi yake.

Fussball Bundesliga FC Bayern München gegen Eintracht Frankfurt
Robert Lewandowski wa Bayern MunichPicha: Lennart Preiss/Bongarts/Getty Images

"Nataka kucheza kandanda na kufunga mabao. Lakini ni kitu cha kawaida kwamba nafarijika, kwamba naweza kufunga mabao, na pia kuweza kushinda. Kwa hivi sasa tunacheza kila baada ya siku tatu, tumo katika wakati muhimu, katika awamu muhimu ya msimu na kila mchezo ni mhimu sana na kila goli liko katika hali hiyo."

Bayern ina pointi 70 kutokana na michezo 28, wakati VFL Wolfsburg inafuatia ikiwa na poiti 60, Borussia Moenchengladbach ina pointi 53 baada ya kuishinda Borussia Dortmund kwa mabao 3-1 siku ya Jumamosi, kipigo kikubwa kwa Borussia msimu huu na ulikuwa ushindi wa wazi kabisa kwa Gladbach, licha ya mshambuliaji aliyeichambua Borussia kama karanga Patrick Herrmann akisita kusema kwamba Borussia msimu huu ni nyanya .

Bundesliga 19. Spieltag Borussia Mönchengladbach SC Freiburg
Patrick Herrmann wa Borussia MoenchengladbachPicha: Dennis Grombkowski/Bongarts/Getty Images

"Hapana, Dortmund ni timu nzuri sana. Hilo wamelionesha pia leo. Lakini nafikiri, lile bao la mapema limetupa karata muhimu. Hii ilikuwa safi sana, kupata bao katika dakika za mwanzo. Na pamoja na hayo tulicheza kwa nidhamu ya hali ya juu, hatukutoa nafasi na katika mashambulizi ya kushitukiza tulikuwa hatari."

FSV Mainz ilipokea kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya Bayer Levekusen , na wakati Schalke 04 ikiwa na matumaini bado ya kucheza katika michuano ya Ulaya ilitoka sare ya bila kufungana na SC Freiburg. FC Kolon ilisherehekea mafanikio makubwa jana Jumapili dhidi ya 1899 Hoffenheim kwa ushindi wa mabao 3-2 na kupata kupumua kidogo ikitumai kuwa kitisho cha kushuka daraja kinapungua.

Fussball Bundesliga Mönchengladbach gegen Borussia Dortmund
Kocha wa Borussia Dortmund akiwa katika tafakuri ya kinaPicha: picture-alliance/AP Photo/Frank Augstein

VFB Stuttgart ilijikakamua kutoka mkiani kabisa mwa ligi na kupanda ngazi moja , na hivyo kufufua matumaini yake ya kubakia daraja la kwanza baada ya kuishinda Werder Bremen jana Jumapili kwa mabao 3-2 katika mchezo ulioshuhudia timu hiyo ikicheza kwa muda wa dakika 7 wakiwa wachezaji kumi uwanjani baada ya Martin Harnik kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano.

Kocha Huub Stevens amezungumzia kuhusu mchezo huo.

"Mchezo kama huo unashangaza. Tena wakati timu inacheza na watu kumi tu na kupata ushindi, mtu hujisikia vizuri. Na tena hali hii inatoa fursa ya kujiamini siku zijazo."

Kocha wa zamani wa Mainz 05 Thomas Tuchel anaripotiwa kuwa anapendelea kujiunga na SV Hamburg , wakati miito imeongezeka leo kwa klabu hiyo kongwe ya Bundesliga ambayo iko mkiani mwa ligi kufanya mabadiliko haraka.

Wakati huo huo Bayer Leverkusen jana Jumapili(12.04.2015) imetangaza kuachana na mlinzi wake kutoka Bosnia Emir Spahic mara moja kutokana kitendo cha mchezaji huyo kumshambulia mlinzi wa uwanjani katikati ya wiki katika mchezo wa kombe la shirikisho kati ya Bayern Munich na Leverkusen ambapo Bayern ilishinda kwa mikwaju ya penalti na kufanikiwa kuingia nusu fainali ya kombe hilo DFB Pokal.

Bayer Leverkusen Spieler Emir Spahic
Mlinzi wa Leverkusen Emir SpahicPicha: picture alliance/dpa/M. Becker

Klabu hiyo ya Bundesliga imesema haina uchaguzi isipokuwa kuchukua hatua hiyo baada ya ushahidi wa video kuonesha Spahic akimshambulia mlinzi mmoja. Leverkusen imesema mkataba wa mchezaji huyo umekatishwa kwa manufaa ya pande zote.

Mwandishi : Sekione Kitojo / ape / dpae / rtre / afpe

Mhariri: Yusuf, Saumu