1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern na mtihani dhidi ya Manchester City

30 Septemba 2013

Kocha wa Bayern Pep Guardiola atakabiliwa na mtihani mwingine dhidi ya timu ya premier League, katika Champions League baada ya kupata ushindi wa kombe la Super Cup dhidi ya Chelsea kupitia mikwaju ya penalti

https://p.dw.com/p/19rkv
Picha: picture-alliance/dpa

Mlinda lango wa Bayern Manuel Neuer anasema huu utakuwa mchuano wa timu mbili zenye nguvu sawa, wakati naye nahodha wa Manchester City Vincent Kompany akiwataka wenzake wakaze buti baada ya kichapo cha mabao matatu kwa mawili dhidi ya Aston Villa.

Katika kundi F, Arsenal ambao maisha yao yanaonekana kuwa ya starehe wakati wakiongoza Ligi Kuu ya England, watakuwa wenyeji wa Napoli. Timu zote mbili zilishinda mechi zao za kwanza za Champions League.

Nao Borussia Dortmund wana mchuano wa nyumbani dhidi ya Olympique Marseille. Baada ya kichapo cha nyumbani cha mabao mawili kwa moja na West Bromwich Albion Jumamosi iliyopita katika Ligi ya nyumbani, mbinyo unazidi kuongezeka dhidi ya kocha wa Manchester United David Moyes kabla ya mpambano wao wa Jumatano ugenini na Shakhtar Donetsk katika kundi A.

Juventus watakuwa wenyeji wa Galatasaray katika mchuano wa kundi B kati ya mabingwa wa Italia na Uturuki, ambao wamemkaribisha Roberto Mancini kama kocha wao mpya. Real Madrid watakuwa nyumbani kupambana na FC Copenhagen, kurejesha ujasiri wao baada ya kunyamazishwa mwishoni mwa wiki katika mchuano wa ligi ya nyumbani waliofungwa bao moja kwa sifuri na Atletico Madrid.

Kevin Prince Boateng ameongeza makali katika ushambuliaji wa Schalke tangu alipojiunga nao msimu huu
Kevin Prince Boateng ameongeza makali katika ushambuliaji wa Schalke tangu alipojiunga nao msimu huuPicha: picture-alliance/dpa

AC Milan inawakaribisha tena kikosini Riccardo Montolivo na Stephan El Shaarawy baada ya kupona majeraha yao pamoja na Mario Balotelli ambaye amepumzika vya kutosha, wakati watakapochuana na Ajax mjini Amsterdam katika mechi ya kundi H hapo kesho.

Barcelona watasafiri mjini Glasgow kupambana na Celtic hapo kesho katika mechi ya kundi H, bila ya huduma za mashambuliaji wao Lionel Messi. Muargentina huyo alipata jeraha katika mguu wake wa kulia mwishoni mwa wiki lakini Neymar yuko tayari kulijaza pengo hilo.

Atletico Madrid watasafiri hadi Porto katika mchuano wa kundi G. Real Sociedad watajaribu kujikwamua ugenini dhidi ya Bayer Leverkusen katika mechi ya kundi A. Schalke wa Ujerumani wako na kibarua dhidi ya Basel katika mechi ya kundi E, baada ya timu hiyo ya Uswisi kubwaga Chelsea mabao mawili kwa moja katika mchuano wa kwanza nao Schalke wakawapiku Steaua Bucharest mabao matatu bila jawabu. Sasa kocha wa Chelsea Jose Mourinho anasema Juan Mata ataanza katika mchezo wa kesho dhidi ya Steaua ambao ni lazima aishinde. Katika kundi C, Paris St Germain watapambana na Benfica nao Anderlecht wakiwaalika Olympiakos siku ya Jumatano.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman