1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich yavunja rekodi nyingine

Admin.WagnerD14 Desemba 2015

Viongozi wa Bundesliga Bayern Munich wametawazwa kwa mara ya tano mfululizo kuwa mabingwa wa majira ya mapukutiko, muda ambao ligi hiyo inakwenda mapumziko

https://p.dw.com/p/1HNJR
Fußball Bundesliga FC Bayern München vs. FC Ingolstadt
Picha: Getty Images/Bongarts/A. Hassenstein

Ligi ya Bundesliga imebakiza mchezo mmoja kwenda mapumziko, ambapo katika mchezo wa 16 mwishoni mwa juma Bayern ilijiimarisha kileleni kwa ,kuishinda Ingolstadt kwa mabao 2-0 na kubakia pointi tano juu ya Borussia Dortmund inayoshikilia nafasi ya pili katika ligi hiyo. Borussia Dortmund ilifanikiwa kujiimarisha katika nafasi hiyo kwa kuishinda Eintracht Frankfurt kwa mabao 4-1 jana Jumapili.

Mlinzi wa Eintracht Frankfurt Bastian Oczipka alizungumzia kuhusu mashabiki wa timu hiyo kuchoma bendera ya klabu kutokana na hasira baada ya kufungwa. "hakuna wakati mzuri tu katika soka. Ni kitu cha kawaida kwa mashabiki kukasirika, kwasababu tumeshindwa. Tunapaswa kujipanga kuhusiana na hali hii. hatuwezi kukimbia kuingia katika vyumba vya kuvalia na kusema , hili halinihusu. Tunapaswa kwenda, na kuwasilikiza mashabiki na kujadiliana nao na hili pia tulilifanya".

Eintracht Frankfurt imeporomoka hadi nafasi ya 15, hali ambayo inamuweka kocha Armin Veh katika hali ya mashaka ya kufungishwa virago. Hata hivyo ulikuwa ushindi wa saba wa Borussia Dortmund mund katika uwanja wake wa nyumbani jana kutoka michezo minane iliyochezwa katika uwanja wa Signal Iduna Park.

Mchezaji wa kati wa Dortmund Ilkay Gundogan amesema kwamba kila kitu kilikwenda vizuri jana. "Tuna kila sababu ya kufurahi. Ulikuwa mchezo mzuri sana kwetu tangu mwanzo. Kwa kweli goli tulilofungwa hatukustahili kufungwa. Lakini tuliendelea tu kucheza vizuri na halikutufanya tusijiamini, tulitengeneza nafasi nzuri za mabao. Kwa jumla ulikuwa naamini , mchezo mzuri kwetu kwa jumla. Na kwa hiyo tunakamilisha mwaka 2015 nyumbani vizuri sana".

Fußball Bundesliga Bayer 04 Leverkusen vs. Borussia Mönchengladbach
Chicharito alisababisha usumbufu katika lango la wageni GladbachPicha: Getty Images/Bongarts/S. Steinbach

Mshangao mkubwa ulitokea siku ya Jumamosi wakati Bayer Leverkusen baada ya kutupwa nje ya Champions League kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Barcelona , hasira zake iliishushia Borussia Moenchengladbach kwa kuishindilia mabao 5-0 na kuweka breki kwa mfululizo wa ushindi wa Gladbach katika Bundesliga msimu huu. Kocha wa Gladbach alizungumzia kipigo hicho cha mbwa mwizi. "Siwezi kucheka kuhusiana na hilo. Ni machungu makubwa na inaumiza. Tumefadhaishwa, bila shaka , kwamba tumeshindwa bila ubishi. Tuliwapa wapinzani fursa ya kutuadhibu, mambo mengi hayakwenda sahihi, hatukuweza kucheza mchezo wetu, leo hatukuweza kupambana kabisa. Na hatimaye tunapata kipigo kama hiki".

Nayo Schalke 04 iliangukia pua pale ilipochapwa mabao 2-1 na Augsburg, ushindi ambao umesaidia timu hiyo kujinasua angalau kwa sasa kutoka katika eneo la hatari la kushuka daraja, na kuchupa hadi nafasi ya 13 katika ligi yenye timu 18.

Mchezaji wa kati wa Augsburg Markus Feulner amesema timu hiyo sasa inaonekana kuwa na usalama. "Utaona kwamba usalama umerejea, kwamba hadi mwisho wa mchezo tunajiamini hadi katika dakika ya mwisho. Na mbele kila mara mmoja wa washambuliaji anaweza kupata bao. Tulipoteza mtiririko wetu wa uchezaji mwanzoni mwa msimu. Sasa kila wakati hali inakuwa mzuri. Utaona kwamba timu sasa inajiamini zaidi. Wachezaji wanafahamu kile wanachotakiwa kufanya. Wana mpango wa wazi, mkakati wa wazi ,na hawataharuki kutokana na mambo fulani yasiyokwenda vizuri uwanjani.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre /dpae / afpe
Mhariri:Yusuf Saumu