1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern kupambana na Barcelona

24 Aprili 2015

Pep Guardiola atapambana na timu yake ya zamani Barcelona baada ya droo ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kuzikutanisha Barcelona na Bayern Munich. Mabingwa watetezi Real Madrid watachuana na Juventus

https://p.dw.com/p/1FEav
Champions League 2012/13 Halbfinale FC Bayern München FC Barcelona
Picha: PIERRE-PHILIPPE MARCOU/AFP/Getty Images

Guardiola amesema ana furaha kubwa kufuatia droo hiyo na anataraji kuwa mchuano huo utakuwa wa kipekee kwake. Amesema watautathmini mchezo wa Barcelona wakati akimiminia sifa kocha Luis Enrique. Akizungumza baada ya droo kufanywa, mchezaji wa zamani wa Bayern Munich Paul Breitner alisema "Lazima tutambue kuwa tutacheza dhidi ya Barcelona na tunajua kuwa lazima tuonyeshe, tucheze katika kiwango bora zaidi, namna tulivyocheza dhidi ya Porto katika kipindi cha kwanza. Tucheze siyo tu kwa dakika 45 lakini kwa dakika 90 na kisha tunaweza kufikiria kutinga fainali. Lakini pia Barcelona lazima wacheze katika kiwango cha juu zaidi".

Barcelona ambao wako katika nusu fainali kwa mara ya saba katika misimu minane, watakuwa nyumbani Camp Nou dhidi ya miamba hao wa Bundesliga katika mkondo wa kwanza mnamo Mei 5 au 6 wakati mchuano wa marudiano uwanjani Allianz Arena wiki itakayofuata.

Infografik Champions League Auslosung Halbfinalspiele 2014/2015 Englisch

Makamu wa rais wa Barcelona Jordi Mestre anasema atua ya nusu fainali haina timu kubwa na ndogo "Utakuwa mchuano mkali sana dhidi ya Bayern Munich na siyo tofauti dhidi ya Real Madrid au Juventus. Tupo katika nusu fainali, hivyo lazima tucheze kwa kujituma na tunataraji kushinda mechi zote. Itakuwa michuano miwili migumu sana, huku wa marudiano ukiwa nyumbani kwa Bayern. Lakini tuko katika hali nzuri, tunataka kushindana katika kiwango cha juu na tuna matumaini ya kutinga fainali".

Guardiola alishinda Kombe la Ulaya kama mchezaji akiwa na Barcelona mwaka wa 1992 na kisha akashinda mataji 14 katika misimu minne kama kocha, ikiwa ni pamoja na Ligi ya mabinhwa mwaka wa 2009 na 2011. Alijiuzulu baada ya Barca kubumburushwa kwa kufungwa jumla ya magoli saba kwa sifuri katika mikondo miwili na Bayern kwenye nusu fainali ya mwaka wa 2013, wakati miamba hao wa Ujerumani walitwaa ubingwa huo.

Wakati huo huo, Madrid lazima waende nchini Italia kwa mkondo wa kwanza dhidi ya viongozi wa Sirie A Juventus wakati wakilenga kuwa klabu ya kwanza kuhifadhi taji hilo katika historia ya Campions League. Mchuano huo ni marudio ya fainali ya mwaka wa 1998, wakati Madrid walishinda moja bila mjini Amsterdam, na timu hiyo ya Uhispania inapigiwa upatu kumzidi nguvu tena mpinzani wake wa Italia. Mkurugenzi wa michezo katika klabu ya Real Madrid Emilio Butragueno alisema wapinzani wao Juventus hawastahili kupuuzwa. "Nina uhakika wachezaji wa Juventus wana motisha kubwa kutinga fainali na wana wachezaji wenye uzoefu. Hivyo walikuwa wakicheza aina hii ya michuano kwa shinikizo kubwa na sidhani kama itakuwa vigumu kwao".

Juve wamefuzu katika nusu fainali yao ya kwanza tangu waliposhindwa kwa mikwaju ya penalti na timu ya AC Milan yake Ancelotti katika fainali ya 2003 uwanjani Old Trafford. Fainali ya mwaka huu itachezwa katika uwanja wa Olimpiki mjini Berlin, hapa Ujerumani mnamo Juni 6.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba