1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern iliyokumbwa na majeruhi yakaza buti

15 Februari 2016

Bayern Munich iliionesha jana Jumapili(15.02.2015)kwamba imo njiani kuvaa taji lake la nne mfululizo la Bundesliga, baada ya kuirarua Augsburg kwa mabao 3-1 katika mchezo ambao Bayern ilitarajiwa kupata usumbufu mkubwa.

https://p.dw.com/p/1HvlH
Deutschland Bundesliga FC Bayern München Unterstützung für Holger Badstuber
Kikosi cha Bayern MunichPicha: Getty Images/Bongarts/A. Hassenstein

Tuanze na Bundesliga Bayern Munich iliionesha jana Jumapili kwamba imo njiani kuvaa taji lake la nne mfululizo la Bundesliga , baada ya kuirarua Augsburg kwa mabao 3-1 katika mchezo ambao Bayern ilitarajiwa kupata usumbufu mkubwa kutoka kwa timu hiyo inayopewa mafunzo na kocha Markus Weinzierl , kwani ndie kocha pekee katika bundesliga ambaye aliwahi kuifunga mara mbili Bayern ikiwa na kocha Pep Guardiola.

Deutschland David Alaba
David Alaba wa Bayern akipambana na Raul Bobadila wa AugsburgPicha: Reuters/M. Dalder

Licha ya matatizo ya wachezaji wake wengi kuwa majeruhi ambapo mlinzi Holger Badstuber aliumia mazoezini, Bayern haikuonesha ishara za kupunguza kasi yake na imeendelea kuongoza kwa pointi nane juu ya msimamo wa ligi hiyo.

Dortmund yang'ang'ania nafasi ya pili

Borussia Dortmund iliendelea kushikilia katika nafasi ya pili kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Hannover 96 na kufungua mwanya wa pointi 13 dhidi ya timu inayofuatia katika nafasi ya tatu Bayer Lecerkusen. Kocha wa Hannover Thomas Schaaf baada ya kupoteza michezo mitano amesema.

"Nafikiri tumeshuhudia mchezo kutoka kwa timu yangu ambao ulikuwa wa mapambano, hisia na tulivyocheza kama timu kama tulivyokuwa tumepanga. Ninachoomba ni kwamba kutokana na uwezo tulioonesha , kiwango hiki kibakie hivi hivi."

Deutschland Henrikh Mkhitaryan
Henrikh Mkhitaryan akishangilia bao la ushindi la DortmundPicha: imago/Jan Huebner

Leverkusen imefika hapo baada ya kuishinda Damstadt kwa mabao 2-1.

Hertha Berlin imeporomoka kutoka nafasi ya tatu hadi nafasi ya nne baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Stuttgart ambayo hivi sasa inaonesha uhai na imepata mafanikio katika michezo yake mitano iliyopita. Mchezaji wa Stuttgart Filip Kostic ameuzungumzia mchezo huo dhidi ya Hertha.

"Nina furaha sana leo kwasababu tumeshinda. Hizi ni pointi tatu muhimu sana . Sasa tumeshinda michezo mitano mfululizo. Haikuwa rahisi , lakini ninafuraha sana na tunaangalia mchezo wetu wiki ijayo na Schalke. Tuna matumaini na tutajaribu kushinda wiki ijayo."

Schalke 04 iko nafasi ya 5 baada ya kupokea kipigo kutoka kwa Mainz 05 cha mabao 2-1 siku ya Ijumaa, wakati Mainz imepanda hadi nafasi ya 6, na Gladbach imeporomoka hadi nafasi ya 7 kutoka nafasi ya nne baada ya nayo kukubali kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya Hamburg SV.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / dpae /zr /
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman