1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bashir akamatwe-Ocampo

Kalyango Siraj14 Julai 2008

Khartoum yalaani hatua hiyo

https://p.dw.com/p/EcPD
Rais wa Sudan Omar Hassan Al-BashirPicha: AP

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai amefikisha ushahidi katika mahakama hiyo na kuomba waranti wa kumkamata rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan kwa kuhusika na mauaji ya halaiki katika mkoa wa Darfur.

Serikali ya Khartoum imekanusha madai hayo,hata hivyo ikasema itaendelea kutafuta suluhu ya mgogoro wa Darfur.

Mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai ya mjini The Hague nchini Uholanzi imepokea rasmi ombi la kutaka kukamatwa kiongozi wa Sudan Omar Hassan al-Bashir,kutokana madai ya mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita pamoja na makosa mengine dhidi ya binadamu katika mkoa wake wa magharibi wa Darfur.

Ombi hilo limetolewa kwa jopo la majaji wa mahakama hiyo na mwendesha mshataka mkuu wa mahakama hiyo Luis Moreno-Ocampo.

Ombi hilo ndio la kwanza la aina yake kutolewa kwa mahakama hiyo la kumtaka kiongozi aliyoko madarakani kutaka kukamatwa na mahakama hiyo.

Hata hivyo Ocampo amesema kuwa ni wajibu wa jopo la majaji kutoa uamuzi unofaa kutokana na ombi lake hilo.

Sudan kwa upande wake imelaani hatua hiyo na kuonya kuwa itatatiza mchakato wa kuleta amani katika mkoa wa Darfur.

Hatua ya kumkamata rais Bashir imelaaniwa ndani pamoja na nje ya Sudan .

Mbali na vigogo wa serikali ya Khartoum kupinga hatua hiyo pia na vyama vya kisiasa vya upande wa upinzani navyo vimelaumu hatua ya sasa ya mwendesha mashtaka mkuu.Msemaji wa chama cha Democratic Union Party DUP,Taj el Sir Mohammed amesemaitaleta picha mbaya Darfur pamoja na maeneo ya kusini mwa nchi hiyo na kutaka ikomeshwe mara moja.

Rais wa Yemen alionya hapo jumapili kuwa hatua hiyo huenda ikawasha moto katika eneo hilo.

Mashirika ya utoaji misadaa katika Sudan yameimarisha ulinzi yakitaraji visa vya ushambuliaji ambavyo vinaweza kuathiri shughuli za kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika eneo la Darfur.

Hata hivyo inasemekana kuwa baadhi ya vigogo wa serikali wamesema kuwa licha ya hatua ya jumatatu ya Ocampo, Khartoum itaendelea kushirikiana na wahusika kuhusu mgogoro wa Darfur.

Mwendesha mashataka anamshutumu rais wa Sudan kwa kwendesha mauaji ya watu wanaofikia laki tatu na pia kutumia ubakaji kama silaha ya maangamizi.Serikali imekanusha hayo.

Na mawaziri wa mashauri ya kigeni wa mataifa ya kiarabu watakutana jumamosi katika kikao cha dharura kuhusu hatua ya sasa ya mwendesha mashtaka mkuu kuhusu kuomba kukamatwa kwa rais Bashir kwa kuhusika na mauaji ya halaiki katika mkoa wa Darfur.