1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barua pepe binafsi zamtesa Hillary Clinton

12 Mei 2016

Utata wa matumizi ya barua pepe binafsi unaomkabili Bi. Hillary Clinton anayetarajiwa kugombea urais kupitia chama cha Democratic, bado unamwandama wakati akiendelea na kampeni zinazoelekea kileleni

https://p.dw.com/p/1ImVZ
USA New York Vorwahlen Hillary Clinton
Picha: Reuters/M. Segar

Machi 14 mwaka 2012, majira ya saa kumi alfajiri, mjini Washington, mnadhimu mkuu wa Hillary Clinton alipata barua pepe kutoka Shirika la la Ujasusi la Marekani CIA ikiwa na kichwa cha habari, SIRI, ikitokea kwa mnadhimu mkuu wa shirika hilo, Dave Petraeus.

Ujumbe huu ni miongoni mwa zaidi ya barua pepe 30,000, pamoja na nyaraka nyingine zilizowekwa hadharani na CIA. Aidha, ni moja ya maelfu ya ujumbe zilizowekwa alama ya SIRI, ambazo kwa sasa zinafanyiwa uchunguzi, hatua inayoweza kufifisha ndoto za Hillary Clinton za kushinda kinyang'anyiro hicho cha urais.

Iwapo Clinton ambaye yupo katika nafasi nzuri ya kuteuliwa kuwa mgombea wa Wademocrats, hatimaye atashtakiwa kwa kushindwa kuhifadhi vema nyaraka za siri, ni wazi kwamba atajikuta katika wakati mgumu zaidi wa kuendelea na kampeni za kuomba kuwa Rais, wakati akihusishwa na utata huo wa kisheria na mashitaka ya kiusalama.

Barua pepe zilizotoka Shirika la ujasusi la marekani, CIA, ni miongoni mwa nyingine 65, zilizowekwa nembo ya SIRI, ambazo pia hazikuhaririwa kwa umakini. CIA ilisema kuzuiwa kwa baadhi ya barua pepe kulihusiana na sababu za kiusalama wa taifa

Kuwekwa hadharani kwa barua pepe alizotuma na alizozipokea Clinton kati ya mwaka 2009 na 2013, kulipelekea Shirila la uchunguzi la Marekani, FBI kuanzisha uchunguzi na kuanza kuwahoji watu wa karibu zaidi na mwanamama huyo, ambaye anapewa nafasi kubwa ya kugombea urais kupitia chama cha Democratic.

Mpinzani wa Clinton katika kinyang'anyiro cha uteuzi wa chama cha Democratic, Bernie Sanders.
Mpinzani wa Clinton katika kinyang'anyiro cha uteuzi wa chama cha Democratic, Bernie Sanders.Picha: Getty Images/J. Sullivan

Uchunguzi wa barua pepe hizo unaendelea

Mills na Huma Abedin ambao ni watu wa karibu na Clinton kwa kipindi kirefu tayari wamekwishahojiwa, wakati waandishi wa habari wa gazeti la Washington Post na Bi. Clinton mwenyewe wakitaraji kuhojiwa hivi karibuni.

"Hakuna aliyewahi kunifikia, lakini nakumbuka mwezi Agusti, katika kipindi kilichopita cha majira ya joto, nililiweka wazi kwamba niko zaidi ya tayari kuzungumza na yoyote, wakati wowote" Alisema Clinton alipozungumza na kituo cha televisheni cha CBS na kuongeza kuwa "nimekuwa nikiwapa moyo wasaidizi wangu wote kujiamini na lolote linalokuja, na ninaamini kwamba hili linakaribia kumalizika".

Uchunguzi wa FBI ambao hata hivyo uwezo wake haujawahi kuridhiwa unakaribia kumalizika. Maafisa wake wanachunguza barua pepe zilizotiwa alama ya SIRI, ambazo ni pamoja na zenye nyaraka za siri kubwa, zinazofikia idadi yake 2000, barua 65 zenye alama ya Siri, na barua pepe nyingine 22 za siri zilizozuiliwa, ambazo zilikutwa katika mtambo binafsi wa kuhifadhi mawasiliano wa Clinton, uliokuwa umehifadhiwa nyumbani kwake, eneo la Chappaqua, New York.

Usalama wa mtambo huo kwa sasa upo chini ya maafisa usalama wa FBI, na uwezekano wake wa kuingiliwa pia unaibua maswali, hasa baada mvamizi wa mitandao kutoka nchini Romania, Marcel Leher Lazar, anayejulikana zaidi kama Guccifer aliyefungwa nchini Marekani, alipokieleza kituo cha televisheni cha Fox kwamba alijaribu mara kwa mara kuingia kwenye mtambo huo wa Clinton, ingawa hakuweza kuthibitisha.

Sheria inazuia kuhifadhi ama kusambaza taarifa za siri kupitia mtandao ambao si salama, kwa kuwa kufanya hivyo kunaweza kukasababisha athari kubwa kwa usalama wa Taifa. Lakini, wakati huo huo, Bi. Clinton amekuwa akisisitiza barua pepe alizopokea na kutuma hazikuwa na alama ya SIRI.

Donald Trump- Mgombea wa Republican anatarajiwa kuchuana na Clinton uchaguzi mkuu wa Novemba 8.
Donald Trump- Mgombea wa Republican anatarajiwa kuchuana na Clinton uchaguzi mkuu wa Novemba 8.Picha: Getty Images/J. J. Mitchell

Hata hivyo sheria za kiusalama hazikuwazuia maafisa wa usalama kufanya shughuli za kiofisi kupitia akaunti binafsi, ingawa utaratibu wa aina hiyo ulipingwa.

Baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo wa FBI, utawasilishwa idara ya sheria, itakayofanya maamuzi ya iwapo kutakuwa na haya ya kumfungulia mashitaka ya uhalifu dhidi ya Bi. Clinton ama la.

Hadi sasa, wachunguzi hao hawajagundua kithibitisho chochote kwamba Clinton alivunja sheria kwa kukusudia, maafisa hao wameliambia Shirika la matangazo ya televisheni CNN.

Kwa upande mwingine, wakati kampeni zikielekea kileleni, chama cha Republican kimeendelea kutumia sakata hilo kama rungu la kumshushia hadhi mgombea huyo anayeongoza kupitia chama cha Democratic.

Kwenye kampeni za Republican, wanaompinga Clinton wameanza kuvaa fulana zenye ujumbe usemao "Clinton afungwe". Mgombea wa chama hicho, Donald trump anachochea kwa kusema Clinton hana heshima, na amekua akimuita kuwa ni laghai na Hakutakiwa hata kuruhusiwa kugombea.

Mwandishi: Lilian Mtono.

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman.