1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barcelona, Real Madrid zatafuta ubingwa

Bruce Amani
17 Mei 2017

Barcelona na Real Madrid walishinda mechi zao jana kumaanisha kuwa kinyang'anyiro cha ubingwa wa La Liga kitaaamuliwa katika siku ya mwisho ya msimu.

https://p.dw.com/p/2d0gy
Spanien Fußball La Liga FC Barcelona - RC Celta de Vigo
Picha: Getty Images/A. Caparros

Neymar alifunga hat trick katika ushindi wa Barca wa 4-1 dhidi ya Las Palmas, wakati Cristiano Ronaldo alifunga mawili katika ushindi wa Madrid wa 4-1 dhidi ya Sevilla.

Matokeo hayo yaliwaacha mahasimu hao wakiwa na pointi sawa, isipokuwa Barca ina faida ya matokeo kati ya timu hizo mbili. Lakini Real wanaweza kuchukua usukani watakapochuana Jumatano dhidi ya Celta Vigo mechi ambayo iliahirishwa mwezi Februari.

Champions League Real Madrid v Atletico Madrid
Picha: Reuters/P. Hanna

Vijana hao wa kocha Zinedine Zidane wanahitaji pointi nne kutoka kwa mechi zao mbili za mwisho ili kutwaa ubingwa bila kujali ya matokeo ya Barca dhidi ya Eibar mwishoni mwa wiki hii. Mechi ya mwisho ya Madrid ni dhidi ya Malaga.

Atletico Madrid ilijihakikishia nafasi ya tatu na tikiti ya moja kwa moja ya Champions LEAGUE baada ya kutoka sare ya 1-1 na Real Betis, wakati Sevilla walipata nafasi ya nne na nafasi ya kucheza dimba hilo kupitia mechi za mchujo.

Sporting Gijon ilikuwa timu ya tatu na ya mwisho kuiaga LA Liga pamoja na Osasuna na Granada. Villarreal, Athletic na Real Sociedad ndizo timu zinazowania nafasi mbili za Europa Legaue.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga