Baraza la Usalama lipitisha azimio juu ya kuunda mahakama ya kimataifa juu ya Hariri | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 31.05.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Baraza la Usalama lipitisha azimio juu ya kuunda mahakama ya kimataifa juu ya Hariri

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura kuunga mkono kuundwa mahakama maalum ya kimataifa kuwahukumu watu wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya aliyekuwa waziri Mkuu wa Lebanon Rafik Hariri mwaka 2005.

Hayati Rafik Hariri

Hayati Rafik Hariri

Nchi wanachama kumi kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zimeunga mkono kuundwa makahama maalum ya kimataifa juu ya Rafik Hariri lakini wanachama wengine muhimu ,Urusi na China hawakupiga kura. Nchi hizo pamoja na Afrika Kusini ,Indonesia na Qatar zimesema kwamba baraza hilo linavuka mipaka ya mamlaka yake, na kuwa linajiingiza katika mambo ya ndani ya Lebanon.

Aliyekuwa waziri mkuu wa Lebanon hayati Rafik Hariri aliuawa miaka miwili iliyopita na tokea wakati huo jumuiya ya kimataifa imekuwa inashughulikia suala hilo. Watu wengine 22 pia waliuawa katika shambulio la bomu lililotegwa ndani ya gari mjini Beirut ambapo Hariri aliuawa.

Sasa ni juu ya Lebanon kuidhinisha hatua ilioyochukuliwa na Baraza la Usalama hadi tarehe 10 mwezi ujao la sivyo baraza hilo litaunda mahakama huru kama jinsi ilivyofanya kuhusiana na Rwanda na Yugoslavia ya zamani.

Akizungumzia juu ya umuhimu wa uamuzi wa Baraza la Usalama ,balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa bwana Jean Marc de la Sabliere amesema kuwa azimio la baraza hilo ni onyo wazi kwa wale wenye nia ya kuiyumbisha Lebanon.

Ni dhahiri kwamba balozi Sabliere ametoa onyo hilo kuilenga Syria. Serikali ya Lebanon pamoja na nchi kadhaa za magharibi zinadai kuwa Syria ilihusika na mauaji ya Hariri. Lakini Syria imekanusha madai hayo wakati wote.

Hatahivyo China ambayo wakati wote imekuwa inahitilafiana na msimao wa nchi za magharibi imeunga mkono haja ya kudumisha utengemavu nchini Lebanon. Balozi wa China kwenye Umoja wa Mataifa bwana Wang amesema kuwa nchi yake inaiunga mkono serikali ya Lebanon katika lengo la kudumisha umoja na amani nchini lakini amesema kuwa azimio la Baraza la Usalama halina manufaa makubwa.

Akizungumzia juu ya azimio la Baraza la Usalama balozi wa Syria amesema azimio hilo linakiuka katiba ya Umoja wa Mataifa.

Balozi huyo amesema kuwa azimio hilo linaweza kuiingiza Lebanon katika vurumai zaidi.

AM.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com