1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la usalama lawaonya waasi wa Darfur

Josephat Nyiro Charo18 Februari 2012

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeyataka makundi yote yenye silaha katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan kufanya mashauriano ya kutafuta amani na serikali ya Sudan.

https://p.dw.com/p/145Ge
Soldaten der Rebellenorganisation «Sudanesische Befreiungsarmee» (SLA) patrouillieren in Muhujariya in Süden der sudanesischen Provinz Darfur (Archivfoto vom 25.04.2005). In der westsudanesischen Region Darfur spielt sich seit 2003 eine Tragödie ab. In dem Konflikt zwischen den rebellierenden Stämmen und der Zentralregierung starben bislang nach Angaben des Auswärtigen Amtes schätzungsweise 300 000 Menschen, über zwei Millionen Menschen mussten fliehen. Ein Friedensabkommen zwischen Khartum und der Rebellenorganisation «Sudanesische Befreiungsarmee» (SLA) vom Mai 2006 wurde bereits einen Monat später von den Aufständischen wieder annulliert. Jetzt hat Verteidigungsminister Jung (CDU) erklärt, Deutschland könnte im Rahmen eines UN-Mandats deutsche Soldaten auch nach Darfur entsenden. EPA/khaled el Fiqi (zu dpa 4462) +++(c) dpa - Bildfunk+++
Waasi wakipiga doria kusini mwa DarfurPicha: picture alliance/dpa

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeonya kuwa pande zote zinazowashambulia raia na kuukwamisha mchakato wa amani huko Darfur zinaweza kuwekewa vikwazo.

Baraza la usalama limeutoa mwito huo katika azimio lililopitishwa bila kupingwa ambalo linarefusha mamlaka ya jopo la wataalamu wanaosimamia utekelezaji wa vikwazo jimboni Darfur hadi Februari 17 mwaka 2013.

Eneo hilo limekabiliwa na mzozo tangu mwaka 2003 lakini mambo yalianza kutulia tangu mwaka 2009. Makundi kadhaa ya waasi yamesaini mikataba ya amani na serikali, lakini makundi mawili makubwa ya Darfur, yakiwemo kundi la Haki na Usawa, JEM, na kundi la Ukombozi wa Sudan, SPLM, hayajatia saini mikataba hiyo.

Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, Daffa-Alla Elhag Ali Osman, amelihimiza baraza la usalama kuyaadhibu makundi ya waasi ambayo hayatajiunga na mchakato wa amani. Alisema waasi waliobakia wanapatikana katika maeneo ya Sudan Kusini, ambayo ilijitenga na kuwa huru tangu Julai mwaka 2011.

Osman alilitolea mwito baraza la usalama kusaidia kuyashinikiza makundi ya waasi yanayokataa kujiunga na juhudi za amani, yakae kwenye meza ya mazungumzo na kushauriana kwa lengo la kufikia suluhisho la mwisho. Alilihimiza baraza hilo kuishinikiza serikali ya Sudan Kusini isiyasaidie makundi yenye silaha yenye ngome zake nchini humo.

Azimio lililoridhiwa na baraza la usalama limesisitiza uungwaji mkono kikamilifu wa juhudi za kufikia suluhisho linalozijumuisha pande zote katika mzozo wa Darfur. Baraza lilieleza masikitiko yake kwamba watu kadhaa wenye mafungamno na serikali na makundi yaliyojihami na silaha, wameendelea kufanya machafuko dhidi ya raia, kukwamisha juhudi za kutafuta amani na kupuuza matakwa ya baraza hilo. Limeelezea pia nia yake ya kuwawekea vikwazo.

Baraza la usalama limeitaka serikali ya Sudan kuondosha amri ya utawala wa hali ya hatari huko Darfur, iruhusu uhuru wa kutoa maoni na ichukue hatua madhubuti kuhakikisha inabeba dhamana kwa uvunjaji wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na mtu yeyote yule.

Mzozo wa Darfur ulianza mwaka 2003 wakati waasi wa asili ya kiafrika walioishutumu serikali ya Sudan, iliyo na idadi kubwa ya warabu kwa ubaguzi, walipojihami na silaha na kuanza mapambano dhidi ya utawala wa Khartoum. Serikali inatuhumiwa kwa kujibu mashambulio hayo kwa kuwatuma wanamgambo wa kiarabu wa Janjaweed kuwaua raia, dai ambalo serikali inalikanusha.

Sudan's President Omar Hassan Ahmad al-Bashir speaks during a press conference in Istanbul, Turkey on 20 August 2008. Chief Prosecutor Luis Moreno-Ocampo of the International Criminal Court (ICC) in The Hague in July requested the court issue a warrant for the arrest of al-Bashir on charges of genocide, crimes against humanity and war crimes in the Darfur region of western Sudan. EPA/TOLGA BOZOGLU +++(c) dpa - Report+++
Rais wa Sudan, Omar Hassan Ahmad al-BashirPicha: picture-alliance/dpa/Montage DW

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu 300,000 waliuwawa na wengine milioni 2.7 wakalazimika kuyahama makazi yao katika mzozo wa Darfur. Mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, mjini The Hague, Uholanzi, imetoa waranti wa kukamtwa rais wa Sudan, Omar Hassan al Bashir, kwa jukumu lake katika uhalifu dhidi ya ubinaadamu katika jimbo la Darfur.

Mwandishi: Josephat Charo/APE

Mhariri: Sekione Kitojo