1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama lashindwa kukubaliana

3 Agosti 2011

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limeshindwa kufikia makubaliano kuhusu msimamo wa pamoja dhidi ya matumizi ya nguvu nchini Syria yaliyogharimu maisha ya watu watatu zaidi jana.

https://p.dw.com/p/129xs
Vikosi vya Syria mjini HamaPicha: picture alliance/abaca

Wanadiplomasia wamesema maendeleo yameweza kupatikana kidogo katika baraza la usalama la umoja wa mataifa jana,,hata hivyo mgawanyiko bado ungalipo miongoni mwa wanachama 15 wa baraza hilo.Wanadiplomasia wanabidi kuwasiliana na serikali zao kabla ya kuendelea na majadiliano baadae hii leo.

Akizungumzia matumizi ya nguvu yaliyokithiri,katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amesema rais Bachar al Assad "amepoteza utu."

Jana mjini Hama,ndugu wawili wa kiume waliuliwa kombora lilipopiga katika gari yao na raia mwengine alifariki dunia baada ya kupigwa risasi na mtu aliyejificha .Habari hizo zimetangazwa na mwenyrkiti wa shirika la haki za binaadam la Syria Rami Abdel Rahmane.

Mapigano yanaendelea tangu majeshi yakisaidiwa na vifaru yalipouvamia mji huo jumapili iliyopita ili kuvunja nguvu maandamano ya upande wa upinzani.

Shahidi mmoja anasema

"Upande wa upinzani unachukua tahadhari,kila wakati tunasikia risasi zikifyetuliwa na watu wasioonekana.Hatujui kama wanawalenga waatu au wanafyetua risasi hewani ili kuwatisha watu wasikusanyike."

UN Sicherheitsrat New York Dossierbild 3
Baraza la usalama la Umoja wa mataifaPicha: cc-by-sa-Patrick Gruban

Shirika rasmi la habari la Syria-Sana limesema "kundi la waharibifu" wamevunja jengo la mahakama huko Hama.Kabla ya hapo shirika hilo la habari lilisema jeshi litaendelea na opereshini zake huko Hama dhidi ya makundi yaliyojiandaa vyema na ambayo yanatumia silaha za kimambo leo.

Kutokana na hali hiyo ndipo baraza la usalama lilipokutana kwa mara ya pili jana baada ya kikao kama hicho kumalizika bila ya matokeo yoyote jumatatu iliyopita.

Urusi na China,mataifa mawili wanachama wa kudumu wa baraza la usalama wametishia kuzuwia azimio lolote,huku Brazil,India na Afrika Kusini wakisema wanapinga azimio au taarifa yoyote.

Madola ya magharibi yamependekeza mswaada mwengine wa azimio kuhusu Syria,lakini wanadiplomasia wanasema hauna tofauti yoyote na mswaada wa awali uliokataliwa miezi miwili iliyopita.

Syrien Proteste anti al-Assad
Maandamano dhidi ya rais Bashar al Assad wa SyriaPicha: picture alliance / dpa

Mjini Washington,wapinzani wa serikali ya rais Bashar al Assad wamemsihi rais Barack Obama amshinikize Bashar al Assad aondoke haraka madarakani na vikwazo zaidi vya Umoja wa mataifa viwekwe dhidi ya utawala wake.

Hata hivyo mijini London na Paris viongozi wanaondowa uwezekano wa jumuia ya kimataifa kupitisha uamuzi wa kijeshi dhidi ya Syria.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Afp/Reuters

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed