1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la usalama la umoja wa mataifa lasisitiza aman Gabon

2 Septemba 2016

Hali nchini Gabon inazidi kuwa ya wasiwasi kufuatia mzozo wa matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Ali Bongo dhidi ya Jean Ping, na tayari Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeelezea kusikitishwa na vurugu hizo.

https://p.dw.com/p/1JulZ
Ali Bongo (kushoto) akiwa na mpinzani wake Jean PingPicha: picture-alliance/dpa/E.Laurent/L.JinMan

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliujadili mzozo huo katika mkutano wa ndani kufuatia ombi la Ufaransa. Kikao hicho kilipokea taarifa kutoka kwa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa eneo la Afrika ya Kati, Abdoulaye Bathily, ambaye anasimamia juhudi za kupunguza athari za mgogoro huo.

Wajumbe wa Baraza hilo wametoa wito kwa wagombea wote pamoja na washirika wao kuwa watulivu na kujizuia kufanya fujo au uchochezi utakaozidi kuamsha chuki zaidi na badala yake waliache suala hilo litatuliwe kwa kuzingatia sheria na katiba. Mbali na kuwataka wananchi wa Gabon na wanasiasa kuwa watulivu, pia Baraza la Usalama limesisitizia kuhusu umuhimu wa wa uwazi na na usawa katika mchakato wa uchaguzi.

Kufuatia vurugu hizo za baada ya uchaguzi, watu watutu wamepoteza maisha na wengine karibu 1,000 wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kujihusisha na vurugu usiku wa baada ya Bongo kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya urais dhidi ya Jean Ping.

Gabun Libreville Ausschreitungen nach Wahlen
Polisi wakikabiliana na wafuasi wa Jean PingPicha: Getty Images/AFP/M. Longari

Umoja wa Ulaya na Ufaransa wametoa wito wa kuwepo kwa uwazi katika mchakato wa kuthibitisha matokeo ya uchaguzi huo. Ufaransa ni mkoloni wa zamani wa taifa hilo dogo na lenye utajiri wa mafuta katika Afrika ya Kati.

Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Francois Delattre, mapema alinukuliwa akisema Baraza hilo linatakiwa kutilia mkazo kwenye hatua ambazo zitakazohakikisha uwazi katika upatikanaji wa matokeo, akiongeza kuwa "kama kungekuwa na hali ya uwazi na usawa pengine Gabon isingeingia katika vurugu."

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa, Jean Marck Ayrault, amesema kuwa nchi yake imesikitishwa sana na kinachoendea nchini Gabon

Wito wa kuachiwa kwa wanaoshikiliwa na polisi

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito wa kuachiliwa kwa watu wanaoshikiliwa na polisi na kuongeza kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia, ikiwa wito wa kuhesabiwa upya kwa kura utaafikiwa.

Kiongozi wa upinzani, Jean Ping, aliyekuwa mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, anapinga matokeo hayo na kusema kuwa Bongo ameshinda kwa udanganyifu na hivyo na anataka zoezi la kuhesabu kura lirudiwe chini ya uangalizi maalum.

Matokeo ya uchaguzi huo yalitangazwa siku ya Jumatano alasiri na kumpatia Bongo ushindi kwa 49.8% ya kura, akifuatwa na Ping aliyepata 48.2 % ya kura, ambapo kura zilizowatenganisha zikiwa 5,594.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/AFP/ DPA

Mhariri: Mohammed Khelef