1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kupoteza hadhi yake

Josephat Charo30 Januari 2008

Baraza la usalama linainyanyasa Iran na Palestina na kuipendelea Israel

https://p.dw.com/p/CzYB
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa katika kikao chake mjini New York MarekaniPicha: UN Photo/Eric Kanalstein

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena linakaribia kupoteza dhima yake huku likijiandaa kuweka awamu ya tatu ya vikwazo dhidi ya Iran lakini wakati huo huo likishindwa kuiwekea masharti ya aina yoyote Israel kwa kuendelea kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Wengi wanauliza ikiwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa bado linastahili kusadikika, amesema Mouin Rabbani, muandishi wa habari anayechangia makala katika jarida la Middle East Report linalochapishwa mjini Washington nchini Marekani. Lakini maswali mengine tete aliyoyataja mwandishi huyo wa habari ni ikiwa baraza la usalama linatakiwa kuendelea kusadikika baada ya kushindwa mara kwa mara kuhakikisha amani na usalamana kuvifumbia macho vitisho dhidi ya amani na usalama na ukiukaji wa haki msingi za mamilioni ya watu.

Ama kweli jazba ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na juhudi zake za kutofanya lolote la maana kukabiliana na hatua ya Israel kuyakalia maeneo ya Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan, kufikia kiasi cha kutotoa kauli angalau dhaifu kuhusu janga la kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, kunaashiria mengi. Ni kimya chenye mshindo mkubwa. Na huu ni mzozo ambao Umoja wa Mataifa ulikuwa na jukumu la moja kwa moja kuusababisha mnamo mwaka wa 1947.

Baada ya siku nne za mashauriano ya faraghani wiki iliyopita, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilishindwa aidha kupata azimio dhidi ya Israel au taarifa ya pamoja isiyo na mafungamano.

Huku Marekani ikitaka taarifa kali inayokosoa mashambulio ya maroketi yanayofanywa na wanamgambo wa kipalestina dhidi ya Israel, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa halikukubaliana juu ya taarifa ya pamoja kuulaani uamuzi wa Israel kuwakaba koo wapalestina katika Ukanda wa Gaza na kukatiza umeme na bidhaa za kiutu.

Mataifa yenye uwezo wa kupitisha maamuzi katika baraza la usalama, ambalo pia lina wanachama 10 wasio na viti vya kudumu, ni nchi tano wanachama zenye kura ya turufu, zikiwemo Marekani,Uingereza, Ufaransa, China na Urusi.

Katika taarifa kali iliyotolewa wiki iliyopita, John Dugard, mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayehusika na haki za binadamu, amesema kitendo cha Israel kinakiuka sheria inayokataza adhabu ya pamoja katika mkataba wa nne wa Geneva kuhusu mizozo.

Pia inavunja kanuni msingi za sheria ya kimataifa kwamba harakati za kijeshi sharti zitofautishe kati ya maeneo yanayolengwa na jeshi na raia. Dugard amezungumzia mauaji ya wapalestina 40 huko Gaza na kulengwa kwa ofisi ya serikali karibu na eneo kulikofanywa sherehe ya harusi ambapo maisha ya raia yalipotea. Hatua ya Israel kuvifunga vivuko vya mpakani inazusha maswali muhimu ikiwa Israel inaheshimu sheria za kimataifa na ikiwa imejitolea kwa dhati katika mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati.

Huku likiwa halina makali dhidi ya Israel kama inavyotokea mara kwa mara kwa sababu ya ulinzi unaopewa taifa hilo la kiyahudi na Marekani, Uingereza na Ufaransa, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linajiandaa kupitisha awamu ya tatu ya vikwazo dhidi ya Iran.

´Kwa baraza hilo kukubali shinikizo la Marekani kuiwekea Iran vikwazo licha ya kutokuwepo na mpango wa nyuklia kutaathiri uwezo wa baraza hilo kuaminika,´ amesema Stephen Zunes profesa wa siasa na maswala ya kimataifa katika chuo kikuu cha San Fransisco nchini Marekani.

Profesa huyo amesema kwa miaka 26 Israel imekuwa ikilikiuka azimio nambari 487 la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linaloitaka iuweke mpango wake wa nyuklia chini ya uchunguzi wa shirika la kimataifa la kuzuia utapakazaji wa silaha za nyuklia, IAEA. Mbali na baraza la usalama kutosema lolote kuhusu swala hilo, limekataa angalau kutishia kuiwekea vikwazo Israel.

Ni kejeli kwamba Marekani inaongoza kushinikiza vikwazo vya Umoja wa Mataifa kuhusu maswala ya nyuklia ikizingatiwa kutokana na mkataba wake wa hivi karibuni na India inakiuka ibara ya 8 ya azimio nambari 1172, inayozitaka nchi zote kuzuia usafirishaji wa teknolojia ambayo kwa njia yoyote ile inaweza kusaidia mpango wa silaha za kinyuklia.

Maazimio mawili yaliyowekwa dhidi ya Iran, kwanza Disemba mwaka 2006 na Machi mwaka jana 2007, yaliitaka Iran isitishe urutuishaji wa madini yake ya uranium na kupiga marufuku kuiuzia silaha Iran na kuzifungia mali za Iran katika taasisi za kifedha za nchini kigeni. LakiniIran imekuwa ikisisitiza mpango wake wa nyuklia ni wa matumizi ya amani na haina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litapoteza heshima yake iwapo litaiwekea vikwazo vingine Iran.