1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama kuijadili Korea Kaskazini

Admin.WagnerD12 Februari 2013

Kitendo cha Korea Kaskazini kufanya jaribio la kinyuklia limezusha mtafaruku katika Jumuiya ya kimataifa. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana kujadili kitendo hicho, ambacho Marekani imekiita cha uchokozi.

https://p.dw.com/p/17cvF
Korea Kaskazini yafanya jaribio jingine la nyuklia
Korea Kaskazini yafanya jaribio jingine la nyukliaPicha: Reuters

Korea Kaskazini imesema imefanikiwa kuzifanyia majaribio zana zake za kinyuklia kwenye kituo chake kilichoko kaskazini. Wataalamu wa Marekani, Japan na Korea Kusini wamesema wamerikodi tetemeko la ardhi lenye kipimo cha kati ya 4.9 na 5.2 katika eneo la kituo hicho.

Shirika la habari la Korea Kaskazi limesema jaribio hilo ni jibu kwa kile lilichokiita kitisho kikubwa cha Marekani kwa usalama wake.

Laana kutoka kila upande

Rais wa Marekani Barack Obama amesema jaribio hilo haliisaidii Korea Kaskazini kuwa salama zaidi. Obama amesema kuwa badala ya kuwa taifa lenye nguvu kama inavyoazimia, Korea Kaskazini imeendelea kutengwa, na kuwatumbukiza wananchi wake katika umasikini mkubwa kwa kuendeleza ukaidi katika kuzitafuta silaha za maangamizi.

Kim Jong-Un, Kiongozi wa Korea Kaskazini
Kim Jong-Un, Kiongozi wa Korea KaskaziniPicha: Reuters

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema inabidi kufikiria vikwazo zaidi kwa serikali ya mjini Pyongyang, kutokana na uvunjifu wake mkubwa wa maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Westerwelle ameitolea wito jumuiya ya kimataifa kuwa na msimamo mmoja kuhusu hatua dhidi ya Korea Kaskazini, na kusema suala hilo litakuwa kwenye ajenda ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya, ambao utaanza Jumatatu. Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe amesema nchi yake imejiandaa kwa lolote.

''Tunatafakari vikwazo vyetu binafsi kwa Korea Kaskazini, na tutachukua hatua zozote kutafuta suluhisho. Vile nimetoa maagizo ya kuwa tayari kwa hali isiotabirika, na kuhakikisha usalama wa watu wetu''. Alisema waziri mkuu wa Japan.

Hata China yaja juu

Hata China ambayo ni mshirika pekee wa Korea Kaskazini imelaani jaribio la nyuklia lililofanywa na nchi hiyo, na imemwita balozi wa nchi hiyo mjini Beijing kwa mashauriano.

Majaribio ya nyuklia ya Korea Kaskazini yamelaani na jumuiya ya kimataifa
Majaribio ya nyuklia ya Korea Kaskazini yamelaani na jumuiya ya kimataifaPicha: Reuters

Katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani na washirika wake wanatarajiwa kuishinikiza China iikemee Korea Kaskazini.

Hata hivyo wachambuzi wanasema kuwa uwezo wa China juu ya Korea Kaskazini una kikomo chake, kwa hofu kwamba utawala wa nchi hiyo unaweza kusambaratika, na kuusogeza ushawishi wa Mareakani karibu na mpaka wake.

Hii ni mara ya tatu kwa Korea kaskazini kufanya jaribio la kinyukila, na mara hii zana zilizojaribiwa ni kubwa kuliko za mara mbili za awali.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/AP/dpa

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman