1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Kitaifa la Syria - Assad lazima aondoke

Martin,Prema/afpe17 Desemba 2011

Baraza la Kitaifa la Syria linalojumuisha makundi ya upinzani ya Syria, SNC, linakutana Tunisia kutayarisha mkakati wenye azma ya kuipindua serikali ya Rais wa Syria Bashar al-Assad.

https://p.dw.com/p/13Uet
Burhan Ghalioun, Professor für Soziologie an der Sorbonne, Leiter des Zentrums für Orientalische Studien in Paris
Kiongozi wa Baraza la Kitaifa la Syria SNC, Profesa Burhan GhaliounPicha: Burhan Ghalioun


Kiasi ya wanachama 200 wa kundi hilo kuu la upinzani, wanahudhuria mkutano huo wa faragha wa siku tatu, nje ya mji mkuu Tunis. Kiongozi wa baraza hilo, Burhan Ghalioun amesema, lengo ni kutafuta njia ya kukomesha kile alichokiita "mauaji yanayoendelea kufanywa na serikali halifu." Amesisitiza kuwa makundi ya upinzani hayana budi kushirikiana zaidi na kuibuka imara kufuatia mkutano huo na kuongezea kuwa wanahitaji haraka, uratibu wa hali ya juu na malengo dhahiri. Amesema, Bashar al-Assad lazima atimuliwe madarakani.

Wakati huo huo, mjumbe wa Tunisia katika mkutano huo, Abdallah Turmani amesema, jumuiya ya kimataifa itaombwa msaada wa kuwalinda Wasyria wanaoshambuliwa, lakini bila ya kuingilia kijeshi. Hawataki kuyatia doa mapinduzi yao ya amani kwa kuruhusu hatua za kijeshi. Mjumbe huyo lakini hakufafanua msaada gani utakaoombwa. Baraza la Kitaifa la Syria limeshaungwa mkono rasmi na Ufaransa na hivyo kupandisha hadhi ya baraza hilo.

Hata Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton mapema mwezi huu, alikutana na wanachama kadhaa wa baraza hilo ikiwa ni pamoja na Burhan Ghalioun.
Baraza hilo likikutana Tunisia, nako Syria maelfu ya watu waliandamana katika miji mbali mbali siku ya Ijumaa, kutoa mwito kwa Umoja wa Nchi za Kiarabu kuchukua haraka hatua za kusitisha umwagaji damu unaoendelea Syria. Kwa mujibu wa kundi la Syria la wanaharakati wa haki za binadamu, hadi watu 10 waliuawa katika mapambano yaliyozuka hapo jana. Umoja wa Mataifa unatathmini kuwa zaidi ya watu 5,000 wameuawa na vikosi vya Syria tangu maandamano dhidi ya serikali kuanza miezi tisa iliyopita nchini humo.