1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza kuu lapiga kura dhidi ya hatua ya Trump Jerusalem

Sekione Kitojo
22 Desemba 2017

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limepiga kura kuhusu azimio linalopinga uamuzi wa Rais Donald Trump kuutambua mji wa Jerusalem kuwa makao makuu ya Israel.

https://p.dw.com/p/2pnkp
USA UN-Generalversammlung  Abstimmung zu Jerusalem-Resolution
Picha: Getty Images/S. Platt

Zaidi  ya  nchi 120 zimekaidi  kauli  ya  rais Donald Trump wa Marekani  jana  Alhamis  na  kupiga  kura  kuunga mkono  azimio  la  baraza  kuu  la  Umoja  wa  Mataifa linalotoa  wito kwa  Marekani  kuachana  na  hatua  yake ya  hivi  karibuni  kuutambua  mji  wa  Jerusalem  kuwa mji  mkuu  wa  Israel.

USA New York - UN Vollversammlung mit dem türkischem außenminister  Mevlut Cavusoglu am Rednerpult
Kikao cha dharura cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu JerusalemPicha: picture-alliance/abaca/A. Hosbas

Trump  alitishia  kupunguza misaada  ya  kifedha  kwa  nchi ambazo  zitapiga  kura  kuunga  mkono  azimio  hilo. Jumla ya  nchi 128 ziliunga  mkono  azimio  hilo, ambalo halilazimishi  kisheria, nchi  tisa  zilipiga , na  35 zilijizuwia kupiga  kura. Nchi  21  hazikupiga  kura.

Kitisho  cha  Trump  kinaonekana  kuleta  athari  kwa  kiasi fulani , ambapo  nchi  nyingi  zilijizuwia  kupiga  kura  na kupuuzia  azimio  hilo ambalo  kwa  kawaida  huhusiana na  maazimio  yanayoihusu  Palestina.

Pamoja  na  hayo, Marekani  imejikuta  ikitengwa wakati nchi  nyingi  za  magharibi  pamoja  na  washirika  wake katika  mataifa  ya  Kiarabu  yalipiga  kura  kuunga  mkono azimio  hilo. Baadhi  ya  washirika hao , kama  Misri, Jordan na  Iraq, wanapokea  misaada  mikubwa  ya  kijeshi   ama kiuchumi  kutoka  Marekani, licha  ya  kuwa  kitisho  cha Marekani  kupunguza  misaada  hakikulengwa  kwa  nchi yoyote maalum.

USA UN-Generalversammlung vor Abstimmung zu Jerusalem-Resolution
Nchi zilivyopiga kura kuhusu hadhi ya Jerusalem Picha: picture alliance/dpa/abaca/M. Elshamy

Kwa Wapalestina ni ushindi

Msemaji  wa  rais  Mahmoud Abbas  wa Palestina inayoungwa  mkono  na  mataifa  ya  magharibi aliita  kura hiyo "ushindi kwa  Palestina." Waziri  mkuu  wa  Israel Benjamin Netanyahu  ameipinga  kura  hiyo.

Mapema  mwezi  huu , Trump  alibadilisha  sera  ya miongo  kadhaa  ya  Marekani  kwa  kutangaza  Marekani kuutambua  mji  wa  Jerusalem  kuwa  mji  mkuu  wa Israel. Mji  ambao ni  eneo  takatifu  kwa  Waislamu, Wayahudi  na  Wakristo, na  kwamba  Marekani itahamishia  ubalozi  wake  katika  mji  huo.

USA UN Botschafterin der USA Nikki Haley
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki HaleyPicha: picture alliance/dpa/AAM. Elshamy

Balozi  wa  Marekani  katika  Umoja  wa  Mataifa  Nikki Haley  ameliambia  baraza  kuu  la  Umoja  wa  Mataifa kabla  ya  kura  ya  jana  kwamba  "Marekani  itaikumbuka siku  hii ambapo  imeshambuliwa  katika  baraza  kuu  kwa ukweli  kwamba  inatekeleza  haki  yake  kama  taifa.

"Tutaikumbuka  wakati  tutakapotakiwa  kwa  mara nyingine  tena  kutoa  mchango  mkubwa  kabisa  kwa ajili ya  Umoja  wa  Mataifa, na  mataifa  mengi  yanakuja kwetu  kutuomba , kama  wanavyofanya  kila  mara , kuchangia  zaidi  na  kutumia  ushawishi  wetu kwa  faida yao,"  amesema balozi  huyo.

Kikwazo cha  amani 

Hadhi  ya  mji  wa  Jerusalem ni  kikwazo  kikubwa  kwa makubaliano  ya  amani  kati  ya  Israel  na  Palestina, ambao  walikasirishwa  na  hatua  ya  Trump.

UN - Francois Delattre
Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa mataifa Francois DelattrePicha: picture-alliance/dpa

Balozi  wa  Ufaransa  katika  Umoja  wa  mataifa  Francois Delattre  amesema  katika  taarifa : "Azimio  hili lililoidhinishwa leo linathibitisha  tu uhalali  wa  sheria  ya kimataifa  kuhusu  Jerusalem." Ufaransa  ilipiga  kura kuunga  mkono  azimio  hilo.

Baadaye  jana Alhamis , balozi  wa  Marekani  katika Umoja  wa  Mataifa  Nikki Haley  ameyataka  mataifa  64 yaliyopiga  kura  ya  hapana, kujizuwia  ama  kutopiga kura  kabisa  kufika katika  ghafla Januari  3 "kuwashukuru kwa  urafiki  wenu kwa  Marekani."

Mwanidshi: Sekione  Kitojo  /Sylvia mwehozi

Mhariri: Saumu Yusuf