1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Banki Kuu ya Marekani yakata riba :0.25%

17 Desemba 2008

Ili kuufufua uchumi,Banki kuu ya Marekani imekaribia kufuta riba kabisa.

https://p.dw.com/p/GHmO
Ben BernankePicha: AP

Banki Kuu ya Marekani-US Federal Bank- jana iliteremsha kiwango cha riba hadi 0.25%.Hiki ni kima cha chini kabisa cha riba kwa mikopo katika historia ya Marekani.Banki Kuu ya Marekani ikatangaza kwamba kila silaha iliopo itumiwe ili kurejesha ukuaji uchumi na kuimarisha bei .

Kwa muda wa sekunde moja hata bingwa wa maswali ya fedha na uchumi wa kituo cha CNN Ali Velshi, alifadhahika akijaribu kuwasomea watazamaji wa kituo hicho uamuzi huo uliopitishwa muda mfupi kabla na Banki kuu ya Marekani.Hatua hii wazi ya kupunguza riba imekuwa sawa na kupunguza riba hiyo kati ya robo% na kuiondosha kabisa (0).

"Na hii si kawaida" -alisema bingwa huyo wa fedha wa CNN ambae tangu miaka mingi amezowea kutangaza kila uamuzi wa Banki Kuu ya Akiba ya Marekani.Akifadhahika, Ali Velshi alimuuliza mwenzake aliekuwa anaongoza vipindi iwapo nae amewahi kujionea hatua sawa na hii ?

Nae alijibu la, hasha.Hata yeye hakuwahi kujionea uamuzi huu usio na kifani.Takriban bila ya kulipa kodi,mabenki mengine ya Marekani yaweza sasa kukopa fedha kutoka Banki Kuu kwa shughuli zao.Banki Kuu ya Marekani imepunguza kiwango cha riba kwa kadiri ambayo mabingwa wachache tu wa fani hii walitazamia.

Wakati huo huo Wakuu wa Banki kuu hiyo wameepusha kuondoa riba kabisa.Mkuu wa Banki Kuu ya Marekani Ben Bernanke akidhihirika kutotoa dhana kwamba ameishiwa na mbinu zake za sera za fedha.Katika vita vya kupambana na kudorora uchumi,mtu hutumia kila mbinu iwezekanayo-alisema Ben.Hii inatokana na kuwa kila kukicha, ununuzi wa bidhaa na utiaji raslimali unapungua na hata uzalishaji mali viwandani.

Isitoshe, hali katika masoko ya kazi inazidi kuwa mbaya :Watu 533,000 walipoteza kazi zao mwezi uliopita tu wa Novemba.Hii ikapelekea idadi kubwa kabisa ya waliomba misaada kwa kupoteza kazi zao tangu kupita miaka 26.Baada ya dhiki si faraji-bali dhiki zaidi, kwani mwakani inabashiriwa hali itakuwa mbaya zaidi.Katika hali hii, rais-mteule Barack Obama asema:

"Silaha za kawaida za kuzuwia kuzorota kwa uchumi zinaanza kutuishia."

Hapo ameingiwa na wasi wasi rais-mteule Obama kwa jicho la hatua ndefu za kupunguza riba za Banki Kuu ya Marekani.Lakini,Banki Kuu hiyo chini ya uongozi wa Ben Bernanke haioneshi wasi wasi hapo na inataja mshale ambao bado unabainisha sura ya masoko ya fedha yalivyo.Banki Kuu kwahivyo, inapanga miezi ijayo kununua hisa za kuitia jeki mikopo ya kunua majumba ili kustawisha upya soko la nyumba na mikopo yake.

Kwa muujibu wa taarifa ya jarida maarufu la maswali ya fedha "WALLSTREET-JOURNAL", Banki Kuu ya Marekani (US CENTRAL BANK), inazingatia kwa mara ya kwanza katika historia yake ya kiasi cha karne moja itatoa akiba zake ili kujipatia fedha zaidi kwa shabaha ya kuyaokoa makampuni ya Marekani yasiporomoke chini. Kwa Rais ajae wa Marekani hali ni wazi kabisa kwamba:

Banki kuu pekee haimudu kubeba mzigo wa msukosuko huu wa uchumi,kwahivyo serikali yake Obama itaanzisha haraka mpango wa kufufua uchumi.Dalili njema imetokeza leo,kwani masoko ya hisa ya Marekani yameitikia uzuri uamuzi wa jana was banki kuu,kwani hisa zimepanda juu.