1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban Ki Moon ziarani Sudan Kusini

Admin.WagnerD6 Mei 2014

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon yuko nchini Sudan Kusini katika juhudi za kuukomesha mzozo ulioikumba nchi hiyo huku viongozi wa Sudan Kusini wakikiuka juhudi za kupatikana amani

https://p.dw.com/p/1BuOx
Picha: Reuters

Ziara hiyo ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa inakuja huku majeshi ya serikali na wapiganaji wa waasi wakiendelea kupambana ili kuudhibiti mji wenye utajiri wa mafuta wa Bentiu.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema Ban Ki Moon amekuwa mara kwa mara akiwataka viongozi wa sudan kusini kutafuta suluhisho la kisiasa na kuyasitisha mapigano ambayo yamewaathiri zaidi raia wasio na hatia.

Ban anatarajiwa kukutana na rais wa Sudan Kusini Salva Kiir katika ziara hiyo ya siku moja na pia atakutana na viongozi wa jamii wanaowawakilisha maelfu ya raia wanaojipatia hifadhi katika kambi za majeshi ya kulinda amani ya umoja wa Mataifa.

Jumuiya ya kimataifa yaongeza juhudi za kuumaliza mzozo

Ziara hiyo ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa inakuja siku chache tu baada ya ile waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry mjini Juba ambako alipewa ahadi na Rais Kiir kwamba atakutana na kiongozi wa waasi Riek Machar ili kutafuta njia ya kuumaliza mzozo huo.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na Rais wa Sudan Kusini Salva KiirPicha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Serikali ya Sudan Kusini imeahidi kuwa mkutano kati ya viongozi hao wawili utafanyika hivi karibuni lakini kufikia sasa Machar bado hajathibitisha iwapo yuko tayari kukutana na hasimu wake Kiir.

Kerry ametishia kuwa Marekani itamuwekea Machar vikwazo na kumchukulia hatua nyingine kali iwapo hatajitolea kukutana na Kiir mjini Addis Ababa kwa mazungumzo ya amani.

Katika mahojiano na jarida moja la Sudan siku ya Jumamosi,Machar alinukuliwa akisema anadhani mkutano wa ana kwa ana na Kiir hautakuwa na tija yoyote.

Mapigano yaendelea Bentiu

Mara ya mwisho Ban alikuwa nchini humo ilikuwa ni wakati wa sherehe za Sudan Kusini kujinyakulia uhuru kutoka kwa Sudan mwezi Julai mwaka 2011 lakini leo yuko nchini humo huku kukiwa na mapigano makali katika mji wa Bentiu ulioko katika jimbo la Unity na pia katika miji mingine katika jimbo la Jonglei.

Waasi wa Sudan Kusini wakisherehekea kuudhibiti mji wa Bor
Waasi wa Sudan Kusini wakisherehekea kuudhibiti mji wa BorPicha: AFP/Getty Images

Waziri wa ulinzi Kuol Manyang amesema majeshi ya serikali yanaudhibiti mji huo lakini kuna mapigano makali yanayoendelea viungani mwa mji huo na kuongeza waasi walizidiwa nguvu baada ya kukabiliwa kwa saa nane.

Mapigano ya Sudan Kusini yamesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kuwaacha mamilioni wengine bila makaazi huku mashirika ya kutoa misaada yakionya kuwa kiasi ya raia milioni moja wanakabiliwa na baa la njaa.

Mazungumzo ya kutafuta amani yanayosimamiwa na jumuiya ya ushirikiano ya nchi za mashariki na pembe ya Afrika IGAD yanaendelea mjini Addis Ababa,Ethiopia bila hatua zozote za kutia moyo.

Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu