1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban Ki Moon atoa onyo kwa serikali ya Somalia

MjahidA14 Agosti 2012

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameonya kuwa visa vya vitisho na ghasia zinaweza kuathiri shughuli nzima ya kuteuliwa kwa bunge la Somalia, kabla ya muda unaokaribia kuisha.

https://p.dw.com/p/15pFI
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: dapd

Wiki ijayo Somalia inatarajiwa kufanya uchaguzi wake mkuu na kuteua Serikali mpya pamoja na bunge jipya la nchi hiyo.

Ban Ki Moon sasa ameliagiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua thabiti dhidi ya mtu yeyote au kundi lolote litakalotaka kuyumbisha hatua ya kupatikana kwa amani nchini Somalia. kwa zaidi ya miongo miwili sasa somalia haijawahi kuwa na serikali imara.

Hatima ya serikali ya mpito nchini Somalia inamalizika Agosti 20 mwaka huu, na ifikapo wakati huo viongozi wanaowakilisha ukoo, kabila na makundi tofauti wanatarajiwa kulichagua bunge litakaloandaa uchaguzi mzima. Lakini katika wiki za hivi karibuni taifa hilo limekubwa na mauaji ya mara kwa mara ya viongozi pamoja na madai ya visa vya rushwa.

Baadhi ya vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Somalia
Baadhi ya vikosi vya Umoja wa Afrika nchini SomaliaPicha: picture-alliance/ dpa

Muakilishi maalum wa Umoja wa Afrika nchini Somalia Boubacar Diarr, amesema hivi maajuzi watu wasiojulikana waliwauwa watu wasaba akiwemo mfanyibiashara na muandishi habari mmoja.

Diarr amesema kumekuwa na ukuaji mkubwa wa visa vya mauaji haswaa yanayowalenga waandishi habari, wafanyibiashara, na viongozi wa kisisasa. Diarr ametaka serikali ya Somalia ianzishe uchunguzi juu ya mauaji haya na watakaopatikana wakabiliwe na mkono wa sheria. Mauaji haya yanahusishwa na ung'ang'anizi wa madaraka wakati huu ambapo muda wa serikali ya mpito unamalizika.

Visa kama hivi ndivyo vilivyoufanya Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Ulaya kuingiwa na wasiwasi juu ya hatima ya nchi hiyo huku waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton akifanya mazungumzo na viongozi wa Somalia wakati alipokuwa ziarani mjini Nairobi, Kenya wiki iliopita.

Baadhi ya athari ya mashambulizi ya kundi la Al shabaab
Baadhi ya athari ya mashambulizi ya kundi la Al shabaabPicha: Reuters

Msemaji wa Ban Ki Moon, Martin Nesirky amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametaka viongozi wa kisiasa wa Somlia, viongozi wa kipindi cha mpito na vyama vingine kuwacha tofauti zao na kuweka mbele matakwa ya raia wa Somalia. Serikali ya mpito ya Somalia imekuwa ikisaidiwa sana na zaidi ya vikosi 15,000 vya Umoja wa Afrika ambao mara kwa mara hupambana na waasi wa kundi la al Shabaab. Taifa hilo pia linakumbwa na visa vya uharamia.

Hata hivyo kundi la al-Shabaab lililo na mafungamano na kundi la kigaidi la Al Qaeda limeapa kuiangusha serikali dhaifu ya Somalia inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi kwa kufanya mashambulizi ya bomu ya mara kwa mara na hata mashambulizi ya kujitoa muhanga.

Tangu kuondolewa madarakani kwa rais wa zamani Mohamed Siad Barre mwaka wa 1991, Somalia haijawahi kuwa na serikali imara na amani katika taifa hilo katika pembe ya afrika bado inayumbayumba.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman