1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bajeti ya Ujerumani kwa mwaka 2008

Zawadsky / Oummilkheir4 Julai 2007

Waziri wa fedha wa serikali kuu anapanga kuondowa nakisi ifikapo mwaka 2011

https://p.dw.com/p/CHBh
Waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani Peer Steinbrück
Waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani Peer SteinbrückPicha: AP

Waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani,PEER STEINBRÜCK anapanga hii leo kuwasilisha mswaada wa bajeti ya mwaka 2008 mbele ya bunge la shirikisho Bundestag,mjini Berlin.Mswaada huo wa bajeti unaashiria matumizi yatakayogharimu yuro bilioni 283 toka yuro bilioni 270 kwa kipindi hiki cha bajeti kinachomalizika.Waziri wa fedha Steinbrück anapanga kuchukua mkopo wa yuro bilioni 13 tuu kufidia pengo litakalotokana na tofauti kati ya kiwango cha fedha zinazoingia kutoka kwa walipa kodi na gharama jumla za serikali kuu.Waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani amedhamiria kuendelea kupunguza kiwango cha mkopo hadi kuondowa kabisa nakisi ya bajeti ifikapo mwaka 2011.

Kwa kuandaa mswaada wa bajeti ya mwaka 2008,waziri wa fedha wa serikali kuu PEER STEINBRÜCK amefungua ukurasa mpya unaotoa matumaini ya kujikwamua toka janga la mikopo inayozidi kuongezeka.Katika makadirio ya wastani ya fedha,mshika hazina mkuu wa taifa anapanga,hadi ifikapo mwaka 2011 kuwasilisha kwa mara ya kwanza bungeni bajeti isiyohitaji mikopo.Waziri Steinbrück anataka kuona mkopo uliorundikizana kwa miongo kadhaa iliyopita, unaanza kulipwa miaka itakayofuatia.

Jambo hilo ni muhimu kwasababu kitaifa sawa na kimaisha hali ni ile ile:Hakuna anaeweza milele kuishi kwa kutumia fedha nyingi zaidi kuliko zile anazopata.Serikali kwa muda mrefu haikua ikitilia maanani ukweli huo.Vyenginevyo tunaweza kusema kwa miongo kadhaa Ujerumani ilikua ikiishi kupindukia uwezo wake.Matokeo yake ,serikali kuu,serikali za majimbo , serikali za miji na bima ya malipo ya uzeeni zilijikuta zikikabwa na madeni yaliyofikia yuro bilioni 1500.

Sehemu kubwa ya madeni hayo yamesababishwa na serikali kuu.Inadaiwa yuro bilioni 900 na wadhamini.Matokeo yake yanatisha.Kwa mfano katika thamani ya kiwango cha riba,ambacho katika bajeti za zamani,thamani yake haikua ikitiliwa maanani,kiwango hicho kilikua cha juu kupita kiasi na kufikia yuro bilioni 40.Takriban kila yuro moja kati ya tano serikali kuu inazokusanya kutoka wa walipa kodi,waziri wa fedha hulazimika kuwalipa wadhamini ili kukidhi masharti ya mzigo wa madeni.Balaa kubwa hilo la kumegua donge la masikini kuwapa matajiri.

Si hayo tuu:enzi za kiwango cha chini cha riba kilichokua kikishuhudiwa miaka ya nyuma,zimeshapita hivi sasa.Gharama zinazotokana na kuongezeka kiwango cha riba ziliigharimu nchi hii yuro bilioni 2.8 za ziada.Makadirio ya kuzidi kuongezeka riba bila ya shaka yanamfanya waziri wa fedha asipate usingizi kwasababu yanatishia kuitumbukiza nchi katika hali ya kufilisika.

Kama katika maisha ya kawaida-jibu la busara ni moja tuu.Taifa lazma lipunguze matumizi.Kwa maneno mengine,raia wanabidi waache kutoa madai makubwa makubwa.Na ikiwa hayo hayatawezekana,basi serikali na bunge hawatakua na njia nyengine isipokua kutia breki.

Lakini upande huo viongozi wanaonyesha kuvuta wakati.Kupungua mzigo wa madeni chanzo chake si kupunguzwa matumizi-hali hiyo imesababishwa na mambo matatu:Kwanza hali nzuri ya kiuchumi imesababisha kumiminika mabilioni ya fedha za makampuni katika makasha ya idara za malipo ya kodi na sababu ya pili ni kupanda kwa kiwango cha kodi ziada za bidhaa.Na sababu ya tatu inatokana na kupungua idadi ya wasiokua na ajira-jambo lililopekea kupungua sana fedha serikali inazotoa kugharimia mashirika ya ajira na wakati huo hujo kuweka akiba ya mabilioni ya yuro.

Waziri wa fedha anataka kuweka fedha hizo-Bora zaidi ingekua angeamua kuwarejeshea fedha hizo walipa kodi.

Hata hivyo lakini la kutia moyo ni kwamba ,mwaka huu na kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1973 ,Ujerumani inakopa fedha kidogo kupita kiasi.Kwa mara ya kwanza ambapo kiwango cha mapato kilikua sawa na kiwango cha gharama ilikua mwaka 1969.