1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Waziri mkuu wa Irak, Nuri al Maliki, aamuru uchunguzi wa madai ya ubakaji ufanywe

20 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCQb

Waziri mkuu wa Irak, Nuri al Maliki, ameamuru uchunguzi ufanywe kufuatia madai ya mwanamke mmoja muamini wa madhehebu ya Sunni kwamba alibakwa na maofisa watatu wa polisi wa Irak alipokuwa akizuiliwa mwishoni mwa juma.

Afisa wa polisi wa cheo cha juu amekanusha madai ya mwanamke huyo, ambayo hayangeweza kuthibitishwa.

Mwanamke huyo wa umri wa miaka 20 amesema shida ilianza wakati maafisa wa polisi walipoivamia nyumba yao katika wilaya ya Amil mjini Baghdad juzi Jumapili wakati mumewe alipokuwa hayupo nyumbani.

Amesema maafisa hao walimkamata kwa sababu ya kuwapikia wapiganaji wa kisunni na kumpeleka katika kituo cha polisi ambako walimshambulia na kumbaka.

Mama huyo amesema aliachiliwa huru baada ya jirani yake kuripoti kwa wanajeshi wa Marekani. Afisa wa usalama wa ngazi ya juu amesema maofisa kadhaa wanahojiwa kuhusiana na hujuma hiyo.

Mashehe wa madhehebu ya Sunni wamekasirishwa na kitendo hicho wakikitaja kuwa uovu unaofanywa na vikosi vya serikali.