1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Uchunguzi kufanywa kuhusu ukanda wa video wa kunyongwa Saddam.

3 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCdk

Serikali ya Iraq imeanzisha uchunguzi kuhusu ukanda wa video ulioonyesha jinsi alivyonyongwa Rais wa zamani wa nchi hiyo Saddam Hussein.

Ukanda huo umesababisha maandamano pamoja na upinzani mkali kutoka kwa Waislamu wa madhehebu ya Sunni ambao ni wachache nchini humo.

Ukanda huo ambao umekuwa ukisambazwa kwenye mtandao tangu siku ya Jumamosi, unaonyesha Saddam Hussein akibughudhiwa na watu walioshuhudia wakati akinyongwa ambao wengi wao ni wa madhehebu ya Shia.

Afisa wa serikali ya Iraq amesema uchunguzi huo utabainisha aliyehusika kupiga picha za ukanda huo.

Waziri Mkuu wa Iraq, Nuri Al-Maliki, ameelezea kwamba amekatishwa tamaa na hali nchini Iraq.

Nuri Al-Maliki ambaye ni wa madhehebu ya Shia aliwaambia waandishi wa habari hana nia ya kuwania muhula wa pili na angetamani kuondoka madarakani kabla ya mwisho wa kipindi anachotawala sasa.