1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD : Mkutano wa Baghdad wafanikiwa

11 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCKD

Iraq imedokeza kwamba mataifa makubwa duniani na nchi jirani ikiwa ni pamoja na serikali ya Marekani na mahasimu wake Iran na Syria yamekubaliana mjini Baghdad kwamba ni muhimu kwa wote kukomesha umwagaji damu wa kimadhehebu usinee katika eneo zima la Mashariki ya Kati.

Lakini wakati Rais George W. Bush wa Marekani hapo jana ameamuru kupelekwa kwa wanajeshi 4,400 zaidi nchini Iraq ziada ya kuongeza kikosi kengine ambacho tayari amekiidhinisha Iran imetowa wito wa kuondolewa kwa vikosi vyote vya Marekani vilioko nchini Iraq kwa hoja kwamba vinachochea umwagaji damu.

Kufuatia mazungumzo ya hapo jana mjini Baghdad kati ya maafisa waandamizi Marekani imesema Uturuki imekubali kuandaa mkutano unaofuatia wa ngazi ya mawaziri hapo mwezi wa April ambapo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice atahudhuria.

Waziri wa mambo ya nje wa Iraq Hoshiyar Zebari ameuelezea mkutano huo wa jana juu ya usalama wa Iraq kuwa wa tija.