1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD : Haijulikani Saddam kunyongwa lini

29 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCfO

Maafisa wa serikali ya Marekani na Iraq wametowa maelezo ya kutatanisha juu ya wakati wa kunyongwa kwa Saddam Hussein.

Afisa mwandamizi wa usalama wa Marekani amesema rais huyo aliengushwa madarakani anaweza kutiwa kitanzi hata hapo kesho Jumamosi.

Lakini maafisa wa Iraq wamejiepusha na madokezo kwamba watamnyonga Saddam kwa hakika katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja waziri mmoja wa serikali ya Iraq ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba sherehe ya kidini ya Idd el Haj itakayodumu kwa wiki nzima itachelewesha kunyongwa kwa kiongozi huyo wa zamani wa Iraq.

Hapo jana Saddam Hussein aliagana akiwa gerezani na kaka zake wawili wa kambo ambapo wakili wake amasema alikuwa katika hali ya uchangamfu na alionekana dhahir kuwa anajiandaa kusubiri kunyongwa.

Amewaambia kaka zake hao wa kambo Watban na Sabawi ambao nao pia wanashikiliwa kwenye kambi ya wanajeshi wa Marekani ya Cropper karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad kwamba alikuwa na furaha kuwa atakabiliana na kifo chake mikononi mwa maadui zake kwa hiyo atakufa shahidi na sio kuozea gerezani.

Pia amewapa ndugu zake hao baruwa kwa familia yake.

Dikteta huyo wa zamani amehukumiwa adhabu ya kifo kuhusiana na mauaji ya Washia 148 hapo mwaka 1982 katika mji wa Dujail kaskazini mwa Baghdad.

Kwa mujibu wa sheria ya Iraq hukumu hiyo lazima itekelezwe katika kipindi kisichozidi siku 30.