1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bado hakuna ishara ya maridhiano mjini Bruxelles

Oummilkhheir22 Juni 2007

Kansela Angela Merkel ameingia mbioni kuwatanabahisha viongozi wenzake juu ya umuhimu wa waraka mpya

https://p.dw.com/p/CB3M
Kansela Angela Merkel
Kansela Angela MerkelPicha: AP

Mnamo siku ya pili ya mkutano tete wa viongozi wa Umoja wa ulaya,kansela Angela Merkel amekua na mazungumzo makali pamoja na rais Lech Kaczynski wa Poland kwa matumaini ya kuwatanabahisha viongozi wa Warsaw wakubali kuunga mkono mswaada wa waraka mpya utakaochukua nafasi ya katiba inayobishwa ya Umoja wa ulaya.

Binafsi kansela Angela Merkel amekiri duru zote za mazungumzo hazikusaidia bado kusonga mbele katika suala la waraka mpya uliolengwa kumaliza miaka miwili ya mzozo unaozikaba taasisi za umoja wa ulaya baada ya katiba kukataliwa kwa kura ya maoni nchini Ufaransa na Uholanzi.

Baada ya mazungumzo yake ya mwanzo jana usiku pamoja na rais Lech Kaczynski,akishiriki pia rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa,kansela Angela Merkel alikua na vikao viwili vya mazungumzo hii leo pamoja na kiongozi huyo wa Poland,kabla ya chakula cha mchana cha viongozi wa mataifa yote 27.Na hata jioni hii kansela Angela Merkel alizungumza baidi na kiongozi huyo wa Poland.

Poland inapinga mfumo wa upigaji kura ujulikanao kama “wingi mara dufu” ikihoji mfumo huo “unaipendelea zaidi Ujerumani.Mfumo huo unataka uamuzi upitishwe ikiwa utaungwa mkono kwa asili mia 55 ya nchi wanachama ambazo wakaazi wake wanafikia asili mia 65 ya wakaazi jumla ya Umoja wa ulaya.

Kwa mujibu wa mwanadiplomasia mmoja wa Poland,pendekezo la rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy la “ufumbuzi wa Ionnina uliofikiwa mwaka 1994,halitoshi.Panahitajika masharti ziada ambayo ni pamoja na kuakhirishwa kutiwa njiani mfumo wa wingi mara dufu wa kura .Kuna wengine nchini Poland wanaodai waraka wa Umoja wa ulaya uakhirishwe hadi mwaka 2020 badala ya mwaka 2009 kama ilivyopangwa.

Duru za Austria zinasema kuna wanaopendelea waraka mpya uanze kutumika mwaka 2014-ikisadif na kuanza kipindi cha bajeti mpya ya Umoja wa Ulaya kati ya mwaka 2014 na 2020.

Mbali na juhudi za kuitanabahisha Poland,kansela Angela Merkel alikua na mazungumzo pia pamoja na waziri mkuu wa Uholanzi Jan Peter Balkenende na waziri mkuu wa Tchek Mirek Topolanek-nchi mbili ambazo pia hazijavutiwa bado na mswaada wa makubaliano uliandaliwa na Ujerumani.

Kansela Angela Merkel alikutana pia na waziri mkuu wa Uengereza Tony Blair,aliyetishia kuzuwia makubaliano yasifikiwe ikiwa madai ya nchi yake hayatazingatiwa kikamilifu.

Licha ya patashika hiyo,waziri mkuu wa Luxembourg Jean Claude Juncker anasema:

“Bado sio mapendekezo yote yaliyofikishwa katika meza ya majadiliano,lakini yapo na yanaweza kuchangia kupatikana makubaliano yatakayoziridhisha pande zote.”

Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya,José Manuel Durao Barroso ameonya waraka mpya usije ukarejesha nyuma sera muhimu za Umoja wa ulaya mfano uhuru wa kushindana kibiashara.

Majadiliano moto moto yanaendelea na wanadiplomasia hawaamini kama maridhiano yatafikiwa kabla ya baadae leo usiku.