1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Azimio la vikwazo vipya dhidi ya Iran lawasilishwa UN

Mataifa makubwa wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamaoja na Ujerumanai yamesema kuwa yamekubaliana juu ya rasimu ya azimio la vipya dhidi ya Iran.

default

Waziri wa Nje wa Marekani Hillary Rodham Clinton

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton alitangaza hayo mbele ya kamati ya baraza la seneti ya nchi hiyo mjini Washington.

Aliiambia kamati ya Mambo ya Nje ya Baraza la Seneti kuwa makubaliano hayo yamefikiwa kwa ushirikiano na Urusi pamoja na China.

"Leo nina furaha kutangaza mbele ya kamati hii, kuwa tumefikia makubaliano kwa kushirikiana na Urusi pamoja na China juu ya rasimu ya azimio dhidi ya Iran.Tunapanga kuwasilisha rasimu hiyo hii leo katika Baraza la Usalama.Na nadhani kuwa tangazo hilo linadhihirisha jibu kwa juhudi zilizochukuliwa mnamo siku chache zilizopita huko Iran, kwa kadri tulivyoweza´´

Hata hivyo Bibi Clinton hakufafanua yaliyomo katika rasimu hiyo ya azimio la vikwazo dhidi ya Iran, hususan kwa serikali na jeshi la walinzi wa mapinduzi ya nchi hiyo Republican Guards.

Lakini mwanadiplomasia mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani amenukuliwa na shirika la habari la Ufaransa AFP akisema kuwa rasimu ya azimio hilo inataka kufanyiwa upekuzi kwa meli zote za Iran, baharini na bandarini.

Amesema kipengele hicho kinafanana na kile kilichomo katika azimio namba 1874 dhidi ya Korea Kaskazini, ingawaje kunatofauti kidogo ya lugha iliyotumika.Azimio hilo dhidi ya Korea Kaskazini lilipitishwa mwaka jana.

Rasimu ya azimio dhidi ya Iran ni matokeo ya kikao cha wiki kadhaa cha mataifa hayo matano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani. Kundi hilo linaundwa na nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi, China pamoja na Ujerumani.

Bibi Clinton amesema mataifa hayo hayakubaliani na mpango uliyosimamiwa na Uturuki pamoja na Brazil, ambapo Iran itapeleka nchini Uturuki sehemu ya madini yake ya uranium kiasi cha tani 1.2 kwa ajili ya kurutubishwa ambapo Uturuki itaipatia nchi hiyo mafuta ya nyuklia.

Balozi wa Brazil katika Umoja wa Mataifa, Maria Luiza Ribeiro Viotti alielezea kutofurahishwa kwa nchi yake na hatua iliyochukuliwa na Marakeni pamoja na washirika wake, na kuongeza kuwa nchi hiyo haitajihusisha kwa namna yoyote katika kuijadili rasimu ya azimio hilo, ikisisitiza kuwa makubaliano yaliyofikiwa na Iran ni hatua muhimu.

Naye mwanadiplomasia mmoja wa Uturuki akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina lake , ameunga mkono kujadiliwa kwa azimio hilo, lakini akasema mwelekeo uwe mwengine kwa kutilia maanani makubaliano ya Iran yaliyofikiwa hapo siku ya Jumatatu.

Susan Rice

Balozi Susan Rice

Lakini Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Susan Rice alisema makubaliano hayo hayahusiani na urutubishaji wa madini ya uranium hatua iliyosababisha kitisho hicho cha vikwazo zaidi dhidi ya Iran.

Hata hivyo Waziri wa Nje wa China, Yang Jiechi alizungumza na mawaziri wenziye wa nje wa Uturuki na Brazil, ambapo aliwaambia China imefurahishwa na kufukiwa kwa makubaliano hayo na kuelezea matumaini yake kuwa yatasaidia kuutanzua mzozo wa mpango wa nyuklia wa Iran kwa njia ya majadiliano.

Mataifa ya magharibi yana wasiwasi na mpango huo wa Iran kuwa ni hatua ya kuelekea katika kutengeneza bomu la nyuklia, kitu ambapo Iran imekuwa ikikanusha na kusisitiza kuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kiraia.

Mwandishi: Ralph Sina

Tafsiri: Aboubakary Liongo

Mhariri: Josephat Charo

 • Tarehe 19.05.2010
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/NRYF
 • Tarehe 19.05.2010
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/NRYF

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com